Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA KUSAFIRISHA CHANGUDOA





WAFANYABIASHARA wawili akiwemo mkazi wa Zanzibar, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka tisa ikiwemo kusafirisha binadamu kwa lengo la kwenda kuwafanyisha biashara ya ngono.

Washtakiwa hao ni Fatma Athumani (24) mkazi wa Kariakoo jijini Dar es Salaam na Juma Hamad (42), mkazi wa Bububu, Zanzibar.

Walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Kwey Rusema. 
 
Mwendesha Mashitaka wa Idara ya Uhamiaji, Method Kagoma alidai kuwa kati ya Desemba Mosi na 31, mwaka jana Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam, washtakiwa walimpokea na kumhifadhi Safia Sabuni kwa lengo la kwenda kumwajiri kufanya biashara ya ngono Dubai.

Shtakiwa la pili, tatu, nne na la tano, ilidaiwa kuwa siku na eneo la tukio la kwanza washtakiwa kwa pamoja waliwapokea na kuwahifadhi, Fatuma Mohamed maarufu kama Aisha Almaa (Kigoma), Farida Said na Mwanahawa Bakari (Tanga), Maria Sanga (Mbeya) na Aziza Salumu (Chamazi jijini Dar es Salaam) kwa lengo la kuwaajiri kufanya biashara ya ngono nchini Dubai.

Katika shitaka la sita, ilidaiwa kati ya Februari Mosi na 22, mwaka jana eneo lisilofahamika, kwa lengo la kudanganya, washtakiwa walighushi hati ya kuzaliwa kwa jina la Safia Sabuni wakionyesha kwamba imetolewa na Wakala wa Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita) huku wakijua siyo kweli.

Kagoma alidai katika shitaka la saba kwamba kati ya Februari Mosi na 22, mwaka jana eneo lisilofahamika washtakiwa baada ya kughushi hati ya kuzaliwa ya Safia Sabuni walionyesha kwamba imelipiwa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku wakijua siyo kweli.

Ilidaiwa kuwa Februari 22, mwaka jana Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, walisababisha Safia, Fatuma ama Aisha, Farida au Maua na Mwanahawa kuwasilisha nyaraka za kughushi kwa ajili ya kuomba hati za kusafiria.

Washtakiwa walikana mashitaka hayo.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. 
 
Hakimu alisema kwa kuwa mashitaka yanayowakabiliwa washtakiwa hayana dhamana, wapelekwe mahabusu hadi Februari 4 kesi hiyo itakapotajwa.


CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com