Hizi ni miongoni mwa baiskeli 104 zilizotolewa na Shirika la Kitanzania lisilo la kiserikali liitwalo Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI ) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI zilizotolewa katika mkoa wa Shinyanga.Shirika hilo limetoa baiskeli 104 katika halmashauri nne za wilaya mkoa wa Shinyanga,ambazo ni halmashauri ya mji Kahama,halmashauri ya Msalala,Ushetu na manispaa ya Shinyanga.
Msaada huo umetolewa na Shirika la AGPAHI kwa ufadhili wa Mfuko wa kusaidia watoto wenye VVU wa watu wa Uingereza (Children’s Investment Fund Foundation UK - CIFF) kwa lengo la kurahisisha kazi kwa watoa huduma ya afya kwa ngazi ya jamii ambao hufanya kazi na shirika hilo kuelimisha jamii kuhusu VVU na UKIMWI.Zoezi la kugawa baiskeli hizo limefanyika Februri 02,2016 na Februari 03,2016.Fuatilia hapa chini matukio katika picha 32 zilizoletwa na Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,ndugu Kadama Malunde
Hapa ni katika ofisi ya mganga mkuu wa halmashauri ya mji Kahama mkoani Shinyanga,kulia ni kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya mji Kahama Dkt Samwel Mwalutambi akiwa na Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa jamii kutoka Shirika la AGPAHI, Cecilia Yona akizungumzia kuhusu msaada huo wa baiskeli.Dkt Mwalutambi alilishukuru shirika hilo kwa kuona umuhimu wa kusaidia watoa huduma za afya kwa ngazi ya jamii na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuhudumia jamii.Baiskeli zilizotolewa katika wilaya ya Kahama ni 84 yaani baiskeli 25 Halmashauri ya Mji Kahama, Halmashauri ya Msalala 32 na Halmashauri ya Ushetu 27 kwa ajili ya watoa huduma ya afya ngazi ya jamii
Kulia ni mwandishi wa habari kutoka Radio Kahama FM, bi Amina Mbwambo akizungumza na msimamizi wa kituo cha Huduma na Matunzo kwa watu wanaoishi na VVU kilichopo katika hospitali ya mji wa Kahama -Dkt John Malulu,ambaye pia alieleza kufurahishwa na shirika la AGPAHI kutoa baiskeli 25 kwa halmashauri hiyo.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Kahama – Dr. Joseph Ngowi akizungumza wakati wa kupokea msaada wa baiskeli 25 zilizotolewa kwa Mji wa Kahama na 10 kwa Hospitali anayoiongoza ya Kahama Mji. Baiskeli hizo zimetolewa na shirika la AGPAHI kwa ufadhili wa Mfuko wa kusaidia watoto wenye VVU wa watu wa Uingereza (Children’s Investment Fund Foundation UK - CIFF).Dkt Ngowi alisema watajihidi kadri iwezekanavyo kuhakikisha kuwa baiskeli hizo kutumika kwa kazi iliyokusudiwa ili kuwarahisishia kazi watoa huduma hiyo ambao hufanya kazi ya kutoa elimu ya VVU na UKIMWI kwa kujitolea.
Pichani ni baiskeli kwa ajili ya watoa huduma ya afya ngazi ya jamii katika halmashauri ya mji Kahama mkoani Shinyanga zilizotolewa na Shirika la Kitanzania lisilo la kiserikali AGPAHI (Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI kwa ufadhili wa Mfuko wa kusaidia watoto wenye VVU wa watu wa Uingereza (Children’s Investment Fund Foundation UK - CIFF).
Watoa huduma ya afya ngazi ya jamii katika halmashauri ya mji Kahama mkoani Shinyanga wakikagua baiskeli hizo kabla wakati wa zoezi la makabidhiano
Msimamizi wa kituo cha Huduma na Matunzo kwa watu wanaoishi na VVU kilichopo katika hospitali ya mji wa Kahama, Dkt John Malulu akikagua baiskeli,kulia kwake ni Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa jamii kutoka Shirika la AGPAHI, Cecilia Yona akitoa maelekezo ya kutunza baiskeli hizo ambapo alisema zitakuwa chini ya watoa huduma hao wa afya na watakuwa wanazitunza na baada ya mradi kumalizika zitakuwa zao lakini ambaye hatatumia kwa malengo yaliyokusudiwa atanyang'anywa na kupewa mwingine mwenye wito wa kufanya kazi
Kila mmoja anakagua ya kwake
Msimamizi wa kituo cha Huduma na Matunzo kwa watu wanaoishi na VVU kilichopo katika hospitali ya mji wa Kahama Dkt John Malulu akikagua moja ya baiskeli hizo
Kulia ni Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa jamii kutoka Shirika la AGPAHI, Cecilia Yona akipitia mkataba wa matumizi ya baiskeli na watoa huduma ya afya ngazi ya jamii Kahama Mji,ambapo miongoni mwa masharti ya mktaba huo ni kutumia baiskeli hizo ajili ya kufuatilia wateja waliopotea katika huduma ya kupata dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARV’s) sambamba na kufuatilia watoto chini miaka miwili, wajawazito, wanaonyonyesha na watoto chini ya miaka 15,pia kusaidia jamii kupata elimu ya VVU na UKIMWI.
Hapa ni katika Zahanati ya Segese katika halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga. Pichani ni watoa huduma ya afya ngazi ya jamii kutoka maeneo mbalimbali ya halmashauri ya Msalala waliojitokeza kupokea msaada wa baiskeli wakipitia mikataba ya matumizi ya baiskeli. Katika halmashauri hiyo, jumla ya baiskeli 32 zimetolewa katika vituo vya (Segese 10, Lunguya 10, Chela 9, Ngaya 2 na Bugarama 2)
Bi Cecilia Yona akiwa na watoa huduma ya afya ngazi ya jamii kutoka maeneo mbalimbali ya halmashauri ya Msalala waliojitokeza kupokea msaada wa baiskeli wakipitia mikataba ya matumizi ya baiskeli.
Bi Cecilia Yona akitoa maelekezo kwa watoa huduma ya afya ngazi ya jamii kutoka maeneo mbalimbali ya halmashauri ya Msalala waliojitokeza kupokea msaada wa baiskeli
Baiskeli zilizokabidhiwa kwa watoa huduma ya afya ngazi ya jamii katika eneo la Segese halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga
Wa pili kushoto ni bi Cecilia Yona akiwaonesha watoa huduma baiskeli watakazozitumia kuwafikia wateja wa majumbani
Kulia ni mtoa huduma ya afya ngazi ya jamii bwana Mwaje Dotto akitafakari jambo na Mviu mshauri kituo cha Segese bwana Kanzaga Fabian ambao kwa pamoja walieleza kufurahishwa na msaada huo kwani awali walikuwa wanatumia gharama kubwa kuwafikia wateja majumbani
Hapa ni katika kituo cha afya cha Lunguya katika halmashauri ya wilaya ya Msalala ambapo watoa huduma ya afya ngazi ya jamii katika eneo hilo walipewa baiskeli 10 kwa ajili ya kuwarahisishia kufanya kazi zao.
Bi Cecilia Yona akiwasisitiza watoa huduma za afya ngazi ya jamii kuhakikisha kuwa wanawafuatilia wateja waliopotea katika huduma ya kutumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI(ARV's) katika eneo la Lunguya ili warudi kwenye huduma badala ya kusubiri miili idhoofike ndiyo waanze kutumia dawa
Bi Cecilia Yona akiwa na muuguzi mkuu katika kituo cha afya cha Lunguya Pili Paulo wakati wa kukabidhi baiskeli kwa watoa huduma katika kituo hicho
Kushoto ni Mwandishi wa habari wa Kahama Fm Amina Mbwambo akifanya mahojiano na muuguzi mkuu katika kituo cha afya cha Lunguya Pili Paulo,ambaye alieleza changamoto kubwa katika kituo hicho ni kupotea kwa wateja kutokana na uwepo wa migodi ya madini katika eneo hilo
Kila mmoja akaondoka na ya kwake,kwa kuwa jukumu la kutunza ni kila aliyechukua,basi wengine wakaanza kujaza upepo baiskeli hizo ili waendelee na kazi ya kuelimisha jamii kuhusu VVU na UKIMWI
Hapa ni katika ofisi za afya za manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga ambako zoezi la kukabidhi baiskeli 20 kwa watoa huduma katika manispaa hiyo limefanyika Februari 03,2016 likiongozwa na Meneja Miradi kutoka AGPAHI , Dkt Gastor Njau
Dkt Njau akizungumza wakati wa kukabidhi baiskeli hizo 20,ambapo alitumia fursa hiyo kuwaomba watoa huduma hao wa afya kutumia baiskeli hiyo kuwafikia watoto wanaoishi na VVU waliopotea katika huduma ya tiba na jamii kwa ujumla kwani dhamira kubwa ya shirika hilo ni kuwahudumia wananchi
Dkt Njau alisema baiskeli hizo zitakuwa mali ya watoa huduma hao ambao watakuwa wanazitengeza pindi zinapoharibika
Kulia ni Meneja Miradi kutoka AGPAHI, Dkt Gastor Njau akisaini mikataba ya msaada wa baiskeli kwa watoa huduma ya afya ngazi ya jamii katika manispaa ya Shinyanga,kulia ni bi Dafrosa Chale Shiluka ambaye ni mratibu miradi kutoka AGPAHI
Zoezi la kusaini mikataba ya matumizi ya baiskeli kwa watoa huduma ya afya ngazi ya jamii katika manispaa ya Shinyanga likiendelea. Manispaa hiyo imepata baiskeli 20 kwa watoa huduma ya afya ngazi ya jamii
Dafrosa Chale Shiluka ambaye ni mratibu miradi kutoka AGPAHI akiwaongoza watoa huduma ya afya ngazi ya jamii katika manispaa ya Shinyanga kujaza mikataba wa makabidhiano ya baiskeli hizo
Dkt Njau akijaribu kuendesha moja ya baiskeli hizo baada ya zoezi la makabidhiano kukamilika
Watoa huduma za afya ngazi ya jamii katika manispaa ya Shinyanga wakiwa wameshikilia baiskeli zao-Picha zote na Kadama Malunde- Malunde1 blog Shinyanga
*********
Shirika la Kitanzania lisilo la kiserikali AGPAHI (Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI limetoa msaada wa baiskeli 104 kwa watoa huduma ya elimu ya VVU na UKIMWI ngazi ya jamii katika halmashauri nne za wilaya mkoani Shinyanga.
Zoezi la kugawa baiskeli hizo limefanyika jana na leo ambapo Halmashauri zilizopata msaada huo ni Halmashauri ya Mji Kahama iliyopata baiskeli 25, Halmashauri ya Msalala baiskeli 32, Halmashauri ya Ushetu 27 na Manispaa ya Shinyanga iliyopata baiskeli 20.
Akizungumza wakati wa kukabidhi baiskeli hizo ,Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa jamii kutoka Shirika la AGPAHI, Cecilia Yona alisema msaada huo umetolewa na Shirika la AGPAHI kwa ufadhili wa Mfuko wa kusaidia watoto wenye VVU wa watu wa Uingereza (Children’s Investment Fund Foundation UK - CIFF) ambao ni moja ya wafadhili wa shirika la AGPAHI
“Mfuko huu wa CIFF unafadhili mradi wa kusaidia kuongeza usajili wa watoto waishio na VVU kupata huduma za tiba na matunzo, hivyo, lengo la ufadhili wa baiskeli hizi ni kurahisisha kazi kwa watoa huduma ya afya kwa ngazi ya jamii ambao hufanya kazi na shirika hili”, alisema Yona.
“Matumaini yetu ni kwamba baiskeli hizi zitatumika kwa ajili ya kufuatilia wateja waliopotea katika huduma ya kupata dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARV’s),kufuatilia watoto chini miaka miwili, wajawazito, wanaonyonyesha na watoto chini ya miaka 15 wanaoishi na VVU pamoja na kuisaidia jamii kupata elimu ya VVU na UKIMWI", aliongeza Yona.
Yona aliwataka watoa huduma wa afya waliopata baiskeli hizo kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa huku akiwasisiza juu ya umuhimu wa kufuatilia wateja waliopotea kwani taifa linapoteza nguvu kazi kutokana na baadhi ya watu waliopata maambukizi ya VVU kutozingatia masharti waliyopewa na wataalam wa afya ikiwemo kuacha kabisa kutumia dawa za ARV’s.
"Bado kuna changamoto ya wateja wetu kuacha kutumia dawa hasa wanapoona miili yao ina nguvu lakini pindi tu miili ikianza kudhoofika hukimbilia hospitali,naomba jamii ibadilike,na kupitia baiskeli hizi mtawafikia wale wote waliopotea katika huduma",alieleza Yona.
Naye Meneja mradi kutoka AGPAHI mkoa wa Shinyanga Dkt Gastor Njau alitumia fursa hiyo kuwataka watoa huduma ya afya majumbani kuwafikia watoto wenye maambukizi ya VVU kwani bado watoto wengi hawajafikiwa na kuamini kuwa baiskeli hizo watazitumia kuwafikia watoto walio wengi zaidi.
Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Kahama Dkt Samwel Mwalutambi mbali na kulishukuru shirika hilo kwa kuwajali watoa huduma ya afya majumbani aliwataka waliopata baiskeli hizo kuzitunza kama zao huku akiahidi uongozi wa wilaya kusimamia baiskeli hizo katika vituo vyao vya afya kwa maslahi ya jamii nzima.
Naye Muuguzi mkuu katika Kituo cha afya Lunguya halmashauri ya Msalala Pili Paulo alisema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni wateja wengi kukatisha huduma hali inayowawia ugumu kuwapata ili warudi katika huduma ya tiba kutokana na eneo lao kuzungukwa na migodi hivyo watu wanakuja na kuondoka katika eneo hilo.
Msimamizi wa kituo cha Huduma na Matunzo kwa watu wanaoishi na VVU kilichopo katika hospitali ya mji wa Kahama, Dkt John Malulu alisema hivi sasa hali ya unyanyapaa kwa wagonjwa wa UKIMWI imepungua ukilinganisha na miaka iliyopita na kilichobaki sasa ni unyanyapaa wa watu binafsi kuogopa kupima afya zao ili kubaini kama wana maambukizi ya VVU au la.
Kwa upande wao baadhi ya watoa huduma ya afya waliopata msaada huo, Stella Paul na Nobert Zephania walisema kabla ya kupata baiskeli walikuwa wanalazimika kutumia gharama zao kuwafikia wateja wao hivyo baiskeli hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuifikia jamii.
AGPAHI ni shirika la kitanzania lisilo la kiserikali linalojishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI,kutoa huduma ya kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,kutoa huduma ya uchunguzi na huduma za awali ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga
Social Plugin