Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro(pichani) amewaonya wanaume hususani wa maeneo ya vijijini, ambao hupenda kuoa wanawake wengine tofauti na wa kwenye ndoa zao,kipindi cha mavuno kuacha mara moja kwa sababu ni kuchezea chakula na kusababisha baa la njaa kuingia kwenye familia zao.
Matiro ametoa onyo hilo kufuatia kuwepo tabia kwa baadhi ya wanaume wa vijijini ambao hupenda kuongeza wanawake wengi pale wanapopata mavuno mengi, na kusahau kuhifadhi chakula cha kujikimu na njaa pale msimu wa kilimo unaporejea na kuanza kuomba msaada serikalini.
Akizungumza juzi kwenye mikutano mitatu ya hadhara na wana kijiji cha Itwangi, Didia na Imesela halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini, Matiro alisema kutokana na mwaka huu kuwa na neema ya chakula, hivyo kwa mwananchi au kijiji kitakacho chezea chakula serikali haitapeleka msaada kwao.
“Mwaka huu angalau inaonekana kuna neema ya wananchi kupata mavuno mengi ya chakula hivyo sitategemea tena kusikia Shinyanga tunakabiliwa na baa la njaa ,cha msingi kinachopaswa ni kuhifadhi chakula angalau kila kaya magunia Matatu na zaidi ili muda wa kilimo utakapo wadia muwe na chakula,” alisema Matiro
Serikali ya Shinyanga tumechoka kila mwaka kutembeza bakuli la kuomba msaada wa chakula hii aibu tunataka tuikatae tuhifadhi vyakula vya akiba, na nyie akina baba muache tabia ya kuongeza wanawake kipindi cha Mavuno mnajiongezea Shida baki na mkeo pangeni mikakati ya kimaendeleo”,aliongeza.
Naye mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Kiomoni Kibamba aliendelea kuwasisitiza wananchi hao kuacha tabia ya kuendekeza kulima mazao ya muda mrefu ambayo ni bahati kuhimili ardhi ya Shinyanga, bali wawe wanalima vyakula vya muda mfupi ambao ni Mtama, choroko, viazi vitamu angalau hata hekali moja moja.
Kwa upande wake afisa kilimo wa kijiji cha Ilola tarafa ya Itwangi Hazina Thomas aliishauri serikali itunge sheria ndogo, ambayo itawapatia nguvu za kuwabana wanaume wanaopenda kuuza chakula chote nyumbani kwake, na kuzitumia pesa kwa matumizi yasiyo rasimi ikiwamo kuoa ovyo na kunywea Pombe.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga
Social Plugin