Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

FAMILIA YAZIKA MAITI BILA MWILI KANDO KANDO YA MTO KILOMBERO





Familia ya dereva wa benki ya CRDB Tawi la Ifakara, Dustan Rwegasira (31) juzi ilifanya ibada ya mazishi kando kando ya Mto Kilombero bila ya kuwapo kwa mwili wa ndugu yao huyo, ambaye hakuonekana kwa siku 10 tangu azame mtoni humo kufuatia ajali ya kivuko.

Kabla ya mazishi hayo, palitangulia ibada ambayo ilifanyika nyumbani kwa wazazi wa 'marehemu', mtaa wa Nyamvisi kata ya Ruaha.

Kivuko cha MV II Kilombero kilizama katika Mto Kilombero Januari 27 kikiwa na abiaria na mizigo, kutokana na kusukumwa hovyo na upepo mkali.

Ndugu, jamaa, marafiki na wafanyakazi wa Benki ya CRDB walikusanyika saa nane mchana kando kando ya mto huo, wakiongozwa na baba mzazi, Francis Rwegasira.

Wengine walioshiriki mazishi hayo ni mkewe Flora Hamadi na baba mkubwa Melchior Muangi. Walitupia majini sanda na baadhi ya nguo za marehemu.

Ndugu hao, jamaa na mafariki walichota pia mchanga kando kando ya mto huo na kuumwaga kwenye maji ikiwa ni sehemu ya mila za kabila la wahaya.

Muangi alisema Serikali inapaswa kuwa na vifaa maalumu vya kupimia hali ya hewa katika maeneo ya vivuko ili kunusuru majanga zaidi yanayoweza kuepukika, kama ambalo limewafanya kumpoteza Rwegasira.

Wakati huo huo, zoezi la kukinasua kivuko cha MV II Kilombero kilichopinduka katika Mto Kilombero tangu Januari 27, linaendelea vyema ambapo sasa kionekana kuibuka nusu.

Mkuu wa kikosi cha uzamiaji na uokoaji kutoka kampuni ya M. Divers Ltd ya Dar es Salaam, Hafidh Seif alisema wamezamisha matanki mawili ya lita 5,000 kila moja na kuyafunga kwa nyaya chini ya kivuko na maji yaliondolewa kwa upepo na kufanya kivuko kilichokuwa kimezama kuibuka nusu.

Alisema wameongeza matanki tisa ya lita 2,000 na 3,000 wakiamini ni lazima kitaibuka chote.

Meneja wa Wakala wa Umeme na Ufundi mkoa wa Morogoro (Temesa), Mhandisi Magreth Mapela alitoa wito kwa wananchi kuwa na subira wakati watalaamu wakifanya kazi ya kuibua kivuko hicho.

Alisema baada ya kuopolewa, kivuko kitachunguzwa kwa kina na wataalamu ili kifanyiwe marekebisho na kurejeshwa majini kuendelea na kazi ya kuvusha watu pamoja na mali zao wakati huu ambao daraja la Mto Kilombero likiendelea kujengwa.

Mapela alisema kivuko hicho kikuubuka chote, watatumia magari matatu, mawili yenye uzito wa tani 25 na jingine lenye uzito wa tani 35, kukivuta kivuko hicho hadi eneo la nchi kavu.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com