Manini Marwa, mkazi wa Kiabakari wilayani Butiama, anatuhumiwa kumtishia hakimu Erick Kimaro kwa bastola mahakamani, baada ya kutoridhishwa na hukumu ya kesi ya maombi ya talaka.
Kesi hiyo ilikuwa ikiamuliwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Kukirango, Wilayani Butiama, Mkoani Mara.
Wazee wa Baraza wa mahakama hiyo Ezibon Daniel na Naftari Mabula, walisema kuwa wakiwa katika eneo la mahakama juzi, mtuhumiwa alimtisha hakimu Kimaro kwa bastola wakati akiendelea na mashauri ya mahakama.
Alisema hakimu alianza na kesi hiyo ambayo ilikuwa ni ya kusoma hukumu baada ya kusikilizwa upande mmoja kutokana na mdaiwa kutofika mara mbili kwa tarehe tofauti.
Mabula alisema mshtakiwa huyo alifika mahakamani siku ya kutoa hukumu ya dai la talaka ambayo ilifunguliwa na mke wa mtuhumiwa, Saada Joseph.
Saada alikuwa anaiomba mahakama kumpatia talaka ya ndoa na pia kumsaidia kumpata mtoto wake wa chini ya miaka mitano, aliyekuwa amechukuliwa na mdaiwa bila idhini yake.
Daniel alisema wakati Hakimu Kimaro akisoma hukumu hiyo, mlalamikiwa Marwa alikuwa akisema mahakamani hapo bila kupewa ruhusa ya kuzungumza, ingawa awali alipewa nafasi ya kujitetea ili ndoa hiyo isivunjwe.
“Hakimu alimweleza mlalamikiwa kuwa haoni sababu za kuendelea kuwa na ndoa kwa sababu haoni amani na pia alimtaka kumleta mtoto huyo hapo mahakamani amkabidhi kwa mama yake mzazi," alisema Daniel na kueleza zaidi:
"Hakimu alisema kuendelea kuishi na mtoto chini ya miaka saba ni kinyume cha sheria ya nchi.”
Mabula alisema hakimu alipomaliza kusoma hukumu, mlalamikiwa alipandwa na hasira na aliingiza mkono mfukoni na kuchomoa bastola.
“Kwa bahati askari polisi walishasogea kabla hajaitoa vizuri mfukoni na kumwamuru anyooshe mikono juu.
"Ndipo waliitoa ile bastola na kuifungua ambapo waliikuta ikiwa na risasi tano ndani yake.”
Alisema kutokana na wananchi waliokuwa katika eneo hilo la mahakama kukimbia, hakimu aliahirisha kesi zote siku hiyo kwa kuwa hakuwa na hamu ya kuendelea kufanya kazi kutokana na kuingiwa na hofu kubwa.
Jeshi la polisi wilayani Butiama limethibisha kumshikilia mtuhumiwa huyo kwa kosa la kuingia na silaha mahakamani; kwa nia ya kutenda kosa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Social Plugin