Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HII HAPA ORODHA YA VYAMA VYA SIASA VILIVYOGOMA KURUDIA UCHAGUZI WA MARUDIO ZANZIBAR



Vyama tisa vya siasa kati ya 14 vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu Zanzibar mwaka jana vimeungana na CUF kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, hadi utakapopatikana mwafaka wa kumaliza mgogoro wa kisiasa.

Mratibu wa umoja wa vyama hivyo, Kassim Bakari Ali alisema jana kuwa vyama hivyo vilikutana Unguja na kupitisha maazimio mawili ya kutoshiriki uchaguzi huo.

Vyama hivyo ni UMD, Jahazi Asilia, Chaumma, UPDP, DP, CCK na ACT Wazalendo. Ushiriki wa vyama vya ADC na CCK bado una utata kutokana na wagombea wake kutangaza kushiriki licha ya vyama vyao kuwa na msimamo tofauti, hali iliyosababisha wagombea hao kusimamishwa.

Vyama ambavyo vimetangaza kushiriki marudio hayo hadi sasa ni CCM, Tadea, TLP, Sau na AFP.

Kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita, Zanzibar imeendelea kuwa kwenye mgogoro wa kisiasa kati ya vyama vikubwa vinavyounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya CUF kususia marudio ya uchaguzi baada ya ule wa awali kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Akitaja maazimio ya vyama hivyo, Kassim alisema wamekubaliana kutoshiriki marudio ya uchaguzi huo hadi mgogoro wa CCM na CUF utakapomalizika na wameunda kamati ya wajumbe 18 ya wenyeviti na makatibu wa kila chama ili kuanzisha meza ya kutafuta suluhu ya mvutano uliopo kati ya CCM na CUF.


“Tutaanza kukaa na viongozi wa vyama hivyo kila upande kujua ni nini hasa hatima ya mvutano huo na tunajikwamuaje,” alisema.
Ali ambaye pia ni mwenyekiti wa Jahazi Asilia alisema mgogoro wa Zanzibar utamalizwa na Wazanzibari wenyewe, hivyo ni vyema viongozi hao wa kisiasa wakajenga uvumilivu katika kutafuta mwafaka.

Alisema tatizo la vyama hivyo siyo kushiriki marudio ya uchaguzi huo tu bali ni kuangalia chanzo na hatima ya mgogoro huo kwa masilahi ya Wazanzibari.

Mwenyekiti wa CCK, Constatine Akitanda aliwaambia waandishi wa habari kuwa uamuzi wa kusimamishwa uanachama kwa mgombea wake wa urais, Ali Khatibu Ali, unakwenda sanjari na kutoshiriki uchaguzi hadi maridhiano ya CUF na CCM yapatikane.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia AFP, Said Soud Said alisema jana kwamba, chama hicho kimekubali kurudia uchaguzi huo.


“Lengo la chama chetu ni kushika dola, sasa tusiposhiriki itakuwaje? Kwanza hatuamini kama CUF haijatendewa haki kwa sababu ni kweli kulikuwa na udhaifu, mfano vurugu za kituo cha kupigia kura cha Matrekta Wawi,” alisema.
Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema kama vyama hivyo viliiamini ZEC katika uchaguzi uliopita, vinatakiwa kuiamini kwenye marudio hayo kwa kuwa hakuna mbadala.


“Naomba wakubali kurudia uchaguzi kwani ‘maji yalishamwagika na kuzoleka haiwezekani... Nani aliyekwenda mahakamani kupinga? Wanachoogopa kurudia ni kitu gani kama walishinda?” alihoji Mrema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com