Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HOFU NA MASHAKA UCHAGUZI WA MARUDIO ZANZIBAR

HOFU na mashaka vimeendelea kukomaa miongoni mwa wanataaluma pia wananchi kutokana na uamuzi wa Chama Cha Wananchi (CUF) kugoma kushiriki marudio ya uchaguzi visiwani Zanzibar.

Wakati CUF ikitangaza msimamo huo uliotokana na kikao chake cha Baraza Kuu tarehe 27 na 28 Januari mwaka huu ikiwa ni baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza kufanyika tarehe 20 Machi mwaka, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza chama chake kushiriki uchaguzi huo.

Hatua ya kutangazwa kurudiwa uchaguzi huo inaelezwa na Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavel Lwaitama kwamba ni haramu na ni uvunjifu wa sheria na kuwa hakuna kifungu cha kanuni kinaruhusu kufutwa kwa uchaguzi.

Dk. Lwaitama amesema kuwa, ZEC isijidanganye kwamba inaweza kufanya uchaguzi kwa amani bila kuwepo kwa CUF kwa kuwa nusu ya Wazanzibari ni wanachama wa chama hicho na pia CUF kuwa na wajumbe ndani ya ZEC.


“Tume iliyosimamia uchaguzi haiwezi kujikosoa yenyewe, awali Jecha alitangaza kuwa, watendaji ndio walioharibu uchaguzi, sasa je, hao watendaji wamebadilishwa? na kama wamebadilisha nani aliyefanya kazi hiyo?” amehoji Lwaitama na kuongeza;
“Wasione wananchi wapo kimya, hawawezi kujua wanafikiria nini au wamejipangaje kwani kitendo cha CUF kususia uchaguzi si kitendo kidogo. Na wala serikali isijidangaje kwa kupitia vyama vidogo, ijiulize vyama hivyo vina mchango gani ndani ya Zanzibar?”

Pia, amesema Serikali inatakiwa kutambua kwamba CUF na CCM zinauwiano , hivyo isichukulie rahisi kwamba uchaguzi utakuwa ni wa amani kwa kuwa wanavifaa vyote vya vita.
Dk. Lwaitama amesema kuwa CCM haina ubavu wa kuingia kwenye uchaguzi bila CUF, na kama wanadhania hivyo basi ni mzaha tu wanaoufanya.
Hata hivyo amesema kuwa, ameshangazwa na kitendo cha Serikali ya Tanzania Bara kuendelea kukaa kimya kuhusu Zanzibar akifananisha kitendo hicho ni sawa na Mbuni kujificha kwenye majani mafupi huku akizani haonekani kumbe anaonekana.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Benson Bana ameonesha hofu kutokana na hatua ya CUF kupuuza tangazo la ZEC la kurudia uchaguzi visiwani Zanzibar.
Bana ambaye ni Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Jamii chuoni hapo ameeleza kuwa, kutoshiriki kwao kumeleta mshindo mkubwa na maswali mengi kwa viongozi wengi na kwamba “serikalia haipaswi kukaa kimya.”

“Hadi sasa bado watu wamebaki na butwaa na kutofahamu nini kinaweza kutokea baada ya CUF kutoshiriki uchaguzi,” amesema.
Wasiwasi uliooneshwa na Dk. Lwaitama pia Prof. Bana unawiana na ule wa Makame Ali Maalim ambaye ni Mkazi wa Bububu viziwani Zanzibar ambaye anasema kuwa, hali ya wasiwasi haiepukiki kwa kuwa, CUF kutoshiriki uchaguzi ni wazi kwamba hautafanyika.
“Huwezi kuingia kwenye uchaguzi hapa Zanzibar bila CUF, kama watalazimisha hivyo ni wazi hakuna atakayekubali. Haya yote yanajenga na uchaguzi uliopita na uliosifiwa na wasimamizi wa nje kwamba ulikuwa ni wa amani na haki,” ameeleza Makame.
Makame anawakilisha idadi kubwa ya Wazanzibari walio na wasiwasi kutokana na mvutano uliopo kati ya CUF na CCM ambapo anasema, kama CCM wangekuwa wameshinda basi mvutano huu usingekuwepo.

“Kinachoonekana hapa kuna wana CCM wamejazwa kiburi na wanasiasa kutoka bara, hawa ujanja wao ni msaada kutoka huko na wanapoambiwa iwe iwavyo watarudi madarakani basi hapa ndio wanajawa kiburi. Sina matumaini kama Zanzibar itabaki salama endapo uchaguzi utafanyika bila ya CUF,” amemema Makame.

Tayari wanasiasa, wanataaluma, jumuiya na wachambuzi mbalimbali wameeleza hofu kuhusu Zanzibar kutumbukia kwenye machafuko zaidi ya yale yaliyotokea mwishoni mwa mwaka 2000 chini ya uongozi wa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.
Miongoni mwa walio na hofu ya vurugu ni pamoja na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAWAZA) kwa kushirikiana na taasisi za Kiislam Zanzibar ambao waliwataka wadau kushughulikia mgogoro wa Zanzibar kwa haraka.

Jumuiya hiyo pia imeonesha hofu ya kuwepo kwa kauli za kibaguzi, uchochezi na uhasama zinazoendelea na kumwomba Rais John Magufuli kushughulikia mgogoro jambo ambalo linaonekana kupuuzwa.

Novemba mwaka jana Asasi za Kiraia Tanzania (AZAKI) waliwataka wanasiasa visiwani humo kukaa na kutatua mgogoro wa kisiasa kwa kuwa, kutokuwepo kwa muafaka kunaweza kusababisha vurugu na hatiamye mauaji visiwani humo.

Hofu ya sintofahamu visiwani humo pia imemgusa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe.
Membe ni miongoni mwa wanasiasa nguli waliojitokeza waziwazi na kupinga uamuzi wa kufutwa kwa matokeo yote ya uchaguzi visiwani Zanzibar akisema dunia inashangaa.
Kutokana na hali hiyo ya mashaka Zanzibar, Mwanasheria wa kujitegemea Fatma Karume amemshauri Dk. Shein kukaa pembeni ili kulinda katiba ya nchi hiyo ikiwa ndio msingi wa kuivusha Zanzibar salama.

“Dk. Shein lazima aondoke kwa kuwa kutofanya hivyo ni kuwanyang’anya Wazanzibari haku yao ya msingi,” amesema Fatma ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume.

Source-Mwanahalisionline

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com