Katibu Mkuu wa shirikisho la soka barani Ulaya Gianni Infatino amechaguliwa kuwa Rais mpya wa shirikisho la soka duniani FIFA katika uchaguzi uliofanyika leo.
Infatino amewashinda wenzake wanne katika uchaguzi uliofanyika kwa awamu mbili baada ya kupata kura 115 ambazo ni zaidi ya asilimia 50 za wajumbe wote 207 walioshiriki uchaguzi huo.
Aliyemfuatia kwa karibu ni Sheikh Salman Ebrahim aliyepata kura 88, huku Prince Ali akipata kura 4, na Jerome Champaigne akiambulia kura 0.
Awali katika awamu ya kwanza Infatino aliongoza kwa kupata kura 88.
Mara baada ya kutangazwa rasmi kuchukua jukumu hilo, Infatino amewashukuru wajumbe wote wa mkutano huo hata wale ambao hawajampigia kura, na kuahidi kuwapa ushirikiano katika kutimiza majukumu yake.
Infatino ameahidi kurejesha heshima ya shirikisho hilo, ikiwa ni pamoja na kuongeza uwazi, na kuomba ushirikiano kutoka kwa wanachama wote wa FIFA.
Aliyekuwa akikaimu kiti hicho Issa Hayatou amemkabidhi kiti hicho Infatino na amemtakia heri katika kutimiza majukumu yake huku akimtaka kuhakikisha kuwa imani ya FIFA inarejea katika uso wa wapenda soka duniani.
Infatino mwenye umri wa miaka 45, ambaye ni raia wa nchi mbili Uswisi na Italia atakalia kiti hicho hadi mwaka 2019.
Rais wa Shirikisho la soka Tanzania Jamal Malinzi ni miongoni mwa wajumbe hao 207 walioshiriki uchaguzi huo wa leo.
Social Plugin