ALIYEKUWA Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika katika Serikali ya awamu ya nne, Steven Wasira, jana nusura atembeze mkong’oto mahakamani.
Wasira alijikuta jaribio lake la kutaka kumpiga na kumnyang’anya kamera mpigapicha wa gazeti la Mwananchi, Michal Jamson likikwama baada ya kushindwa kumkamata.
Tukio hilo la aina yake lililovuta hisia za watu wengi waliokuwa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, lilitokea jana saa 5 asubuhi wakati Wasira alipotoka ndani ya mahakama hiyo baada ya ombi la wapigakura wake watatu kupewa ruhusa ya kupinga ubunge wa Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) kutupwa.
Baada ya kutoka ndani ya mahakama hiyo, Wasira aliye maarufu kwa jina la utani la ‘Tyson’, alikutana na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali wakiwa nje wanamsubiri ambapo alizungumza nao.
Lakini baada ya mpigapicha huyo kufika na kuanza kutekeleza majukumu yake, Wasira alionekana kukereka na kutaka kumkamata kwa lengo la kutaka kumpora kamera.
HALI ILIVYOKUWA
Dalili za Wasira kumsaka mpigapicha wa Mwananchi zilianza kuonekana eneo la Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza saa 3:29 asubuhi kabla ya kuelekea jengo la Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara.
Baada ya kubaini uwepo wa mpigapicha huyo, alimfuata na kumhoji ni chombo gani anachofanyia kazi au anatoka mtandao gani wa kijamii, ambapo alimjibu kuwa ni mpigapicha wa gazeti la Mwananchi.
Hatua hiyo ilimfanya Wasira atafakari kwa muda kabla ya kuamua kuingia ndani ya jengo la Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikiliza uamuzi wa kesi ya wananchi watatu waliomba kukata rufaa ya kupinga ubunge wa Bulaya.
Baada ya dakika 25 kupita, mahakama ilitoa uamuzi kuhusu maombi ya wapigakura hao, lakini Wasira alibaki ndani kwa dakika kadhaa, na kutuma wapambe wake kuangalia kama waandishi wa habari wameondoka eneo hilo.
Baadaye Wasira alitoka nje na wapigapicha wakaanza kutekeleza majukumu yao kitendo kilichosababisha arudi ndani.
Akiwa ndani hakukaa muda mrefu, akatoka tena nje, na moja kwa moja akamfuta Jamson, huku akihoji sababu za yeye kupigwa picha.
“We kijana njoo hapa usikimbie, unafanya nini hapa muda wote? Nimekuona muda mrefu unanifuatilia,” alisema Wasira huku akimsogelea kutaka kumkamata na kumnyang’anya kamera yake.
Mpigapicha huyo alipohisi hatari, aliamua kukimbia na Wasira alijaribu kumkimbiza bila mafanikio.
Baada ya kushindwa jaribio hilo, Wasira ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM, aliamua kwenda katika gari lake dogo aina Toyota Mark X lenye namba za usajili T 399 DBG.
Alipanda ndani ya gari hilo pamoja na mmoja wa wapigakura wake waliofungua kesi ya kupinga ubunge wa Bulaya, aliyetambulika kwa jina la Janes Ezekiel.
Hatua hiyo iliwafanya wanahabari waliokuwa nje ya jengo la mahakama kupigwa na butwaa na ghafla waliona gari la Wasira likibadili mwelekeo na kuelekea kwa kasi eneo walipokuwa wamesimama.
Hali hiyo ilisababisha waandishi wa habari kukimbia ili kukwepa gari hilo lisiwagonge.
KAULI YA WASIRA
MTANZANIA lilipomtafuta Wasira kwa njia ya simu ili kujua sababu ya uamuzi wake wa kutaka kumpiga mpigapicha huyo, alisema kuwa alitaka kujua sababu za kumfuatilia kila eneo na hata kumpiga picha alipotoka msalani.
“Nashangaa hapakuwa na waandishi ila yeye tu,” alisema Wasira huku akimtaka mwandishi aliyempigia simu aonane naye ana kwa ana na kisha kukata simu.
RUFAA YATUPWA
Awali kabla ya tukio hilo, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilitoa uamuzi kuhusu maombi ya kukata rufaa yaliyowasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa wapigakura wa Jimbo la Bunda ambao ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagila waliokuwa wakiwakilishwa na mawakili Denis Kahangwa na Costantine Mtalemwa dhidi Mbunge Bulaya, Msimamizi wa Uchaguzi jimbo hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akisoma uamuzi huo wa Jaji Sirilius Matupa, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Eugenea Rujwahukwa, alisema baada ya kutolewa uamuzi wa kutupiliwa mbali kesi hiyo Januari 25, mwaka huu, wapigakura hao hawakuridhishwa, hivyo kuwasilisha tena maombi ya kwenda Mahakama ya Rufaa.
Alisema katika maombi hayo, mawakili wa wapigakura, Mtalemwa na Kahangwa waliomba kufungua shauri Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ili itoe ufafanuzi kuhusu haki ya mpigakura ya kuhoji matokeo na ni vigezo gani vinatakiwa vitimizwe ili mpigakura aweze kuhoji matokeo ya uchaguzi.
Rujwahukwa alisema katika hatua za usikilizwaji wa maombi hayo, wakili wa Serikali, Kidando, alileta pingamizi kuwa maombi hayo hayaendani na sura ya 141 sheria ya rufaa kifungu 15(2) na 1(2) ambapo licha ya mabishano hayo Jaji Matupa alikubaliana na sura hiyo.
“Jaji amekubaliana na sura 141 ya sheria ya rufaa na maombi haya ni ya msingi chini ya kifungu 15(a)(b), lakini yalipaswa kuwa chini ya kifungu 15(c) ambacho ndiyo sahihi kwa ajili ya maombi kama haya, hivyo mahakama imeyatupilia mbali maombi haya ya rufaa kwa ajili ya uimarishaji wa haki na kwamba bado wanayo nafasi ya kuleta maombi mengine ndani ya muda wakizingatia vifungu hivyo vya sheria,” alisema Rujwahukwa.
Januari 25, mwaka huu, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mohamed Gwae, aliitupilia mbali kesi namba moja ya kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la Bunda Mjini iliyofunguliwa na wapigakura hao kwa sababu waleta maombi hakuwa na mamlaka kisheria.
MWAKA 1998
Mwaka 1998, Wasira alidaiwa kumpiga Mhariri Mkuu wa gazeti la Hoja, Sadick Yassin nje ya Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), baada ya gazeti hilo kuandika kichwa cha habari ‘Swahiba wa Mrema aanzisha chama kuiondoa CCM madarakani’.
Wasira hakufurahishwa na neno ‘swahiba’ kwa madai kuwa ni tusi, wakati huo akiwa mwanzilishi wa chama cha upinzani cha National Development Congress (NDC) ambapo alikuwa mwenyekiti.
Katika tukio hilo, Wasira anadaiwa alimpiga ngumi mhariri huyo kisha kumkimbiza hadi ndani ya ofisi za Serikali, huku waandishi wakongwe Raphael Hokororo na Mayage S. Mayage wakishuhudia tukio hilo.
Baada ya tukio hilo, Wasira alijisalimisha Kituo cha Polisi cha Kati kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana ambako alihojiwa kutwa nzima.
Baada ya mahojiano kukamilika, siku iliyofuata alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako kesi yake iliendeshwa kisha kufutwa baada ya walalamikaji kutohudhuria mahakamani.
NA JUDITH NYANGE-MTANZANIA MWANZA
Social Plugin