Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Jipu Limeiva!! ASKARI POLISI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA RUSHWA,ALIOMBA LAKI 7 AMWACHIE HURU MTUHUMIWA



Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Katavi imemfikisha mahakamani askari wa jeshi la polisi wa kituo cha polisi cha Mwese Wilayani Mpanda Peter Kashuta G,451PC ambaye alishawishi kuomba rushwa ya Tsh 700,000 ili aweze kumwachia huru mtuhumiwa.

Mtuhumiwa huyo alifikishwa jana kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda na kusomewa mashitaka na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Bahati Haule mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Chiganga Ntengwa.

Mwendesha mashitaka huyo alidai mahakamani hapo kuwa TAKUKURU Mkoa wa Katavi walipata taarifa kutoka kwa Ruchege Mambalo aliyewekwa mahabusu katika kituo cha polisi Mwese kwa tuhuma za kumpiga mtoto wake aitwaye Lutobhisha Mambalo mwenye matatizo ya akili alipotaka kumchoma kisu baba yake, katika harakati za kujiokoa alichukua jiwe na kumpiga nalo usoni.

Baada ya kupigwa na jiwe hilo alikimbia na kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi Mwese ndipo Ruchega Mambalo alimfuata mtoto wake kituo cha polisi na alimkuta kituoni hapo akiwa na askari Polisi Peter Kashuta ambaye alimshawishi na kumwomba Rushwa ya Tsh 700,000 ili kumwachia huru.

Mwendesha mashtaka huyo wa Takukuru alidai kuwa baada ya kupokea taarifa hizo za askari kuomba rushwa na walianza kufanya uchunguzi wa kina ili kuweza kuthibitisha tuhuma hiyo na ilithibitika na ndipo mtego wa Rushwa uliandaliwa .

Aliiambia Mahakama baada ya mtego kuandaliwa hatimaye Takukuru walifanikiwa kumkamata askari wa Jeshi la polisi Peter Kashuta akipokea rushwa ya Tsh 100,000 kutoka kwa Ruchege Mambalo ili kumfutia tuhuma ya kumjeruhi mtoto wake.

Hahati Haule aliiambia Mahakama kuwa tukio la kukamatwa kwa mtuhumiwa lilitokea Februari 10 huko katika Kijiji cha Lwega kata ya Mwese kwenye mgawaha .

Mshitakiwa alisomewa mashitaka mawili na mwendesha mashitaka huyo wa Takukuru Bahati Haule shitaka la kwanza kuomba na kushawishi rushwa ya Tsh 700,000 na shitaka la pili kupokea rushwa ya Tsh 100,000 kinyume na matakwa ya mwajiri wake kwa mijibu wa kifungu cha sheria 15 kidogo cha kwanza (a( cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 7 yamwaka 2007.

Baada ya kusomewa mashitaka mtuhumiwa alikana mashitaka hayo na Hakimu mkazi Chiganga Ntengwa alimwachia kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja mwenye hati ya nyumba au fedha tasilimu shilingi milioni mbili na kutosafiri nje ya Mkoa wa Katavi bila kibali cha mahakama ya Wilaya ya Mpanda.
 
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com