KUNA HII STORI MPYA KUHUSU BABU WA LOLIONDO,SASA WATANZANIA NA DUNIA NZIMA WATARAJIE MAFURIKO MENGINE




Baada ya kimya cha muda mrefu, Mchungaji mstaafu, Ambilikile Masapila (82) maarufu kama ‘Babu wa Loliondo’, ameibuka upya na kuwataka Watanzania wajiandae kwa ‘mafuriko’ ya watu watakaomiminika nyumbani kwake kutoka katika mataifa mbalimbali duniani, kufuata huduma itokanayo na muujiza mkubwa zaidi kulinganisha na ule wa tiba ya kikombe uliomtokea mwaka 2009.

Akizungumza juzi katika mahojiano maalum na Nipashe nyumbani kwake Samunge, Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Masapila alisema kwa mara nyingine, Watanzania wajiandae kupokea habari njema kuhusiana na muujiza mkubwa wenye kuleta suluhisho la matatizo mengi ya binadamu, na hivyo kulitangaza jina la nchi yao (Tanzania) kote ulimwenguni.

'Babu' alisema ujiuo wa ‘mafuriko’ hayo ya watu utaanza hivi karibuni na ameshaanza maandalizi kabambe ya kupokea ugeni huo utakaokuwa wa kihistoria.

Hata hivyo, Babu Masapila hakutaja ni lini hasa ataanza kutoa huduma hiyo itokanayo na muujiza mpya, bali alisisitiza kuwa “ni hivi karibuni”, hasa atakapokuwa amekamilisha maandalizi ya mahala pa kupokea wageni.

“Nilipata maono ya jambo hili mwishoni mwa mwaka uliopita (2015). Ni ndoto inayohusiana na habari njema kwa binadamu, ni ndoto iliyonilazimu kuanza maandalizi ya kupokea watu wengi zaidi na ndiyo maana nimeanza maandalizi,” alisema Babu Masapila, anayesisitiza kuwa yeye hupata nafasi ya kuzungumza na Mungu (wake) mara kwa mara kupitia ndoto.

Anasema kila anachokifanya hutokana na maagizo anayoyapata kupitia sauti kutoka kwa Mungu.

Hadi kufikia mwaka 2011, Babu Masapila alikuwa gumzo nchini na nje ya mipaka kutokana na huduma yake ya tiba ya kikombe iliyovutia maelfu ya watu.

Dawa hiyo aliyodai inatibu maradhi mengi yakiwamo ya kisukari, aliitoa kupitia kikombe na kuiuza kwa Sh. 500 tu.

Iliwateka watu wa kila namna wakiwamo wanasiasa, viongozi wa kidini, wasanii maarufu, wafanyabiashara na wakuu wa vikosi mbalimbali vya majeshi.

Inakumbukwa kuwa miongoni mwa vigogo waliowahi kufika kwa Babu na kupata ‘kikombe’ ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Rais John Magufuli, ambaye baada ya kunywa dawa aliwaambia watu waliojazana eneo hilo kwa maelfu kuwa serikali itatumia Sh. bilioni 1.05 kutengeneza barabara inayoingia kijijini hapo ili kurahisishia usafiri kwa watu wanaokwenda kwa Babu Masapila.

Wengine waliowahi kufika ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na Askofu Thomas Laizer ambaye sasa ni marehemu.

Ingawa watu waliomiminika kwake mwaka 2011 kwa ajili ya kupata tiba ya ‘kikombe’ walitengeneza msururu mrefu wa magari uliofikia kilometa 15, Babu Masapila alisema watu watakaokwenda kwake sasa kutokana na muujiza mpya watakuwa wengi maradufu na ndiyo maana ameanza kujenga nyumba za kutosha ndani ya eneo lenye ukubwa wa eka 70 ili kuwapokea.

“Kupitia ndoto hiyo niliagizwa kutafuta eneo kubwa na kujenga nyumba za kutosha kwa ajili ya kupokea wageni kabla ya kuanza kutoa huduma," alisema Babu Mwasapila katika mahojiano.

"Nashukuru uongozi wa kijiji (cha Samunge) umenielewa na kuniunga mkono kwa kunipatia eneo nililoelekezwa kwa kazi hiyo (kupitia ndoto).”

Akieleza zaidi, Babu Masapila alisema sauti kupitia ndoto yake ilimuelekeza kujenga nyumba za kupokea wageni katika eneo la jirani na Mlima wa Makao na hivyo, anaushukuru uongozi wa serikali ya kijiji kwa kumpatia eka 70 hizo kandoni mwa mlima huo na tayari ameanza ujenzi wa nyumba hizo.
“Namshukuru sana Mungu. Ana mpango maalumu na Tanzania kupitia Samunge. Naona Tanzania inakwenda kuwa maarufu barani Afrika kupitia Samunge.

"Kutafanyika miujiza mingi na dunia nzima itaijua Tanzania, tena kuliko ule muujiza wa kikombe.“

Babu Mwasapila ni mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Akieleza zaidi maandalizi hayo ya kupokea ugeni mkubwa zaidi, Babu Masapila alisema tayari kuna nyumba sita ameshazijenga na ziko katika hatua ya mwisho ya kukamilika.

Alisema kazi hizo zinarahisishwa na malori mawili aina ya Fuso aliyoyanunua kitambo kwa shughuli za kubeba mchanga na vifaa vya ujenzi, na pia kubebea kuni za kuchemshia dawa zake.

Aidha, gari lake la kutembelea aina ya Toyota Land Cruiser hutumika pia kwa shughuli za kubebea dawa mbalimbali za uponyaji.

Babu Masapila anasema hivi sasa amewaajiri watu 13 ambao huwalipa mishahara kuanzia Sh.100,000 kwa mwezi ili kusaidia maandalizi hayo.

Masapila alisema tangu alipopata maono kuhusu maandalizi ya kupokea ugeni wa watu wengi zaidi, kila anapolala huona makundi ya watu waliosongamana pembeni mwa Mlima Makao na ndiyo chanzo cha kuliomba eneo hilo.

Diwani wa Kata ya Samunge, Kajulus Steven, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, anakiri kijiji kumpatia Babu Masapila eneo la eka 70, kandoni mwa Mlima Makao ili afanye maandalizi kwa ajili ya kuwapokea wageni.

Alisema walimpa eneo hilo baada ya Babu Masapila kuwaeleza kuwa kuna muujiza mwingine hivi karibuni.
“Tulishajifunza kutokana na kile kilichotokea mwaka ule… alituambia anaona watu wakifurika Samunge lakini sisi hatukujali, tukapuuza maono yake.

Mwishowe watu wakafurika kweli, tukahangaika sana,” alisema Steven na kuongeza:

“Kwa sababu hiyo, safari hii tumemsikiliza na kumpatia eneo alilodai kuoteshwa kuwa ndilo linalofaa kwa huduma.
"Viongozi wa eneo hili tulikaa na kuingia naye makubaliano kuwa akimaliza kutoa huduma zake hizo tutalirejesha.”

Steven alisema wanamchukulia Babu Masapila kama ‘nabii’ kwa sababu mambo mengi aliyowahi kutabiri kuwa yatatokea, yametokea kweli, ikiwamo kupata umeme ambao hivi sasa umewafikia kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), na kufikishwa kwa huduma za simu za mkononi baada ya kufungwa kwa minara ya kampuni mbili.

HIVI SASA HALI IKOJE?
Akizungumzia hali ya utoaji huduma za uponyaji hivi sasa kulinganisha na vile ilivyokuwa wakati wa ‘mafuriko’ yaliyotokana na tiba ya kikombe, Babu Masapila alisema ipo tofauti kubwa.

Alisema wakati huo, watu aliokuwa akiwapatia kikombe walikuwa wakifika hadi 18,000 kwa siku lakini hivi sasa idadi hiyo imepungua hadi kuwa chini ya watu 20 kwa siku.

“Hivi sasa nawahudumia (watu) 10 hadi 20 na kwa sababu kila mmoja hulipia Sh. 500, mwanzoni fedha zilizopatikana zilifikia hadi Sh. milioni tisa kwa siku… lakini hivi sasa kiasi kinachopatikana ni kati ya Sh. 5,000 na 10,000,” alisema.

Akieleza sababu za kupungua huko kwa wateja, Babu Masapila alisema hashangazwei kwa sababu anaamini kuwa huo ni mpango maalum wa Mungu.

“Sishangazwi. Mungu mwenyewe amependa kusitisha umaarufu wa huduma hii (tiba ya kikombe) ili nipate muda wa kufanya maandalizi kwa ajili ya kuwapokea watu wengi zaidi watakaofika hapa (Samunge) kuliko wale wa awali,” alisema Babu Masapila.

FAMILIA, HISTORIA
Babu Masapila aliiambia Nipashe kuwa yeye ni baba wa watoto wanne, kati yao watatu ni wa kiume na kwamba, hivi sasa familia yake bado iko Babati mkoani Manyara.

Alisema kabla ya kufika Samunge, alikuwa wilayani Rungwe, mkoani Mbeya. Mwaka 1952 aliondoka (Mbeya) na kwenda Korogwe mkoani Tanga kabla ya kuhamia Babati na kisha kutua Samunge alikokuwa akifanya kazi ya uchungaji wa KKKT.

Alisema baada ya Mungu kumpa nguvu ya uponyaji kupitia kikombe, sasa bado anaendelea kutoa huduma hiyo kwa watu mbalimbali, wengi wanaoendelea kufika kwake wakitokea Dodoma na nchi za Kenya, Uganda, Sudan Kusini na Eritrea.

HALI KIMAISHA
Baada ya kufika nyumbani kwa Babu Masapila na kuonyeshwa mahala anapoishi sasa na pale alipokuwa akiishia awali kabla ya mwaka 2011, mwandishi alibaini kuwa Babu Mwasapila ameimarika zaidi kiuchumi.

Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa awali alikuwa akiishi katika nyumba ndogo ya udongo lakini sasa anaishi kwenye nyumba kubwa na ya kisasa huku pia akitembelea Land Cruiser na kumiliki malori mawili aina ya Fuso, achilia mbali muonekano wake unaoshiria kuwa ni mtu mwenye afya tele.

Aidha, Babu ana mradi wake wa ujenzi wa nyumba sita za kisasa na miundombinu mingine kwa maandalizi ya kupokea maelfu ya wageni kwenye eneo la eka 70.

Mbali na malori yake kumsaidia katika shughuli za maandalizi ya ujenzi wa nyumba za kupokea wageni, pia vyombo hivyo huvikodisha kwa shughuli za ujenzi na hivyo kumuongezea kipato kinachotumika kuboresha huduma zake.

UJIO WA VIONGOZI, WANASIASA
Kuhusiana na namna alivyojisikia baada ya kupata ugeni wa viongozi mbalimbali mashuhuri na watu kutoka nje ya nchi kufuata tiba yake ya kikombe, Babu Masapila alisema hayuko tayari kuzungumzia hilo kwani siyo vizuri kujadili majina ya wale waliowahi kupata huduma yake.

Hata hivyo, alisema anafurahi kuona kuwa wapo wakubwa wengi wanakubali tiba ya kikombe chake na kuiamini kwani ndiyo msingi wa kupona kwa kila anayepata huduma hiyo.

MTI WA DAWA
Akiuzungumzia mti wa dawa ya kikombe, Babu Masapila alisema siyo mpya na wengi wanaufahamu kwa majina taofauti.

“Mti wa dawa ninaotoa unajulikana kwa majina tofauti kulingana na makabila husika. Wairaqw wanauita Titiwi, Wakurya wanaita Mkarakara na Wamasai wanauita Ngamriaki," alisema.

"Siyo kwamba mimi nimeubuni na sikujua kama unatibu, hapana. Mungu aliweka neno na akanionyesha mimi… mtu akinywa kikombe kimoja tu anapaswa kupona.”

Hata hivyo, aliongeza kuwa kama mtu hajapona vizuri, hazuiwi kurudia kunywa kikombe, lakini kwa sharti kwamba siyo kwa siku hiyo bali siku nyingine, hasa baada ya kupita siku saba zinazopaswa kuwa za uponyaji.

Alisema mhusika anapaswa kwenda kupimwa kama maradhi yanayomsumbua yameisha ama la ndani ya kipindi cha miezi mitatu hadi minne.

Alisema wapo baadhi ya watu humpuuza na kumdharau, lakini hilo halimsumbui ila anawasamehe na kumuachia Mungu kwani anajua kuwa wengi wa wanaombeza ni waganga wa jadi wanaohofia kupoteza wateja, na wakuu wa makanisa ya baadhi ya madhehebu ambao huhofia kupoteza waumini wao wenye nia ya kuombewa ili wapate nafuu ya matatizo mbalimbali ya kiafya.

TUHUMA ZA KUSABABISHA VIFO
Babu Masapila alisema anatambua kuwa baadhi ya watu wanaompinga huvumisha kuwa dawa ya ‘kikombe’ chake ilisababisha vifo.

Akielezea kuhusu hilo, alisema hakuna ukweli bali wapo baadhi ya wagonjwa walifariki baada ya ndugu zao kuwatorosha kutoka katika hospitali mbalimbali walikokuwa wamelazwa, na kuzidiwa wakati wakiwa kwenye foleni ya kupata kikombe cha dawa.

“Wengi kati ya wale waliobahatika kupata kikombe walipata nafuu na afya zao kuimarika,” alisema.

Hata hivyo, haitashangaza kusikia kuwa wapo pia watu waliokunywa dawa ya kikombe chake na bado wakafariki dunia, alisema Babu Masapila, kwani yeye hana dawa ya kuzuia kifo.

Alisema hata kwenye hospitali zote duniani wapo watu hupona na wengine hufariki kwa sababu Mungu ndiye huamua hatma ya maisha ya kila binadamu.

Alisema wakati watu walipokuwa wakifurika kwake kufuata tiba ya ‘kikombe’, kuna wataalamu waliojitambulisha kuwa wanatoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali walifika na kuchukua sampuli ya dawa na kwenda kuifanyia utafiti na hakukuwa na majibu yaliyodai dawa hiyo ina madhara.

Babu Mwasapila alisema kuwa wataalamu hao walifika tena na kuchukua mizizi ya mti anaoutumia kwa maelezo kuwa wanakwenda kuchunguza ili kujua ni baada ya muda gani dawa hiyo huua virusi na vimelea vingine vya magonjwa mbalimbali baada ya mtu kuinywa.

“Cha kushangaza, watu hao hawajarudi tena kwangu… kwa hiyo sijui kinachoendelea.”

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kata ya Samunge, Simon Dudui, watu 52 walifariki dunia wakati wakiwa kwenye foleni ndefu kusubiri huduma ya ‘kikombe cha babu’ mwaka 2011.

MATUNDA YA ‘KIKOMBE‘ SAMUNGE
Diwani Steven wa Kata ya Samunge, alisema huduma ya kikombe cha Babu Masapila ilileta maendeleo makubwa na ya ghafla kwao, hasa kuhusiana na barabara, upatikanaji wa maji safi na pia kuinuka kiuchumi kwa baadhi ya wakazi wake.

Alisema kabla ya kikombe cha babu, Samunge hakukuwa na mahala pa kulala wageni na yeyote anayehitaji huduma hiyo alilazimika kwenda Loliondo ambako ni mbali, lakini sasa hali ni tofauti kwani tatizo hilo halipo tena.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Samunge, Jonath Kilobei, alisema ‘kikombe cha babu’ hawatakisahau kwani kimewainua kimaisha kutokana na biashara walizokuwa wakifanya wakati watu walipofurika na kwamba sasa, wanasubiri kwa hamu ujio wa mkubwa zaidi wa wageni kama Babu Masapila alivyowaahidi.

Afisa Mtendaji Dudui, alisema mbali na maandalizi binafsi ya Babu Masapila, wao pia wameanza maandalizi ya kupokea maelfu ya watu kwa kuimarisha huduma za zahanati yao ya Samunge kwa kuipanua na pia kuongeza madaktari wawili.

“Pia kijiji kimetenga eneo la ujenzi wa vyoo na stendi kwa ajili ya kuingiza magari mengi kwa wakati mmoja,” alisema.

Aidha, aliongeza kuwa tayari kijiji cha Samunge kimeanzisha vikundi vya ulinzi na usalama na pia kununua matanki kadhaa ya maji yenye ujazo wa lita 1,000 kila moja ili yasambazwe kwenye maeneo yaliyo karibu na eneo la Babu.

“Hatutaki tena aibu ya wakati ule wa ujiuo wa watu wengi. Tulikuwa tunafanya kazi kwa zimamoto baada ya kupuuza maelezo ya Babu. Hivi sasa tupo naye karibu na tumejipanga mapema kupokea watu wengi zaidi,” alisema Afisa Mtendaji huyo.

Mmoja wa wafanyabiashara wa Kijiji cha Samunge, Aden Sinodia Gibaseya, alisema yeye ni miongoni mwa watu walionufaika kibiashara wakati wa muujiza wa ‘kikombe cha babu’ kwa kuuza maji na vyakula.

Mfanyabiashara mwingine aitwaye Sam Alen Ndugai, alisema naye ni miongoni mwa watu walionufaika sana kwa kuuza vyakula na maji na alikuwa akiingiza hadi Sh. milioni 28 kwa siku.

Hata hivyo, anasema alipata pigo kubwa baadaye wakati shehena ya maji aliyokuwa akiyauza Sh. 4,000 kubaki mikononi mwake kufuatia umati uliokuwa ukifika Samunge kila uchao kupotea ghafla.

“Babu alisisitiza kwamba tusiuze bidhaa zetu kwa bei kubwa. Wengi hatukumsikiliza… tukawa tukiuza chupa moja ya maji kwa Sh. 4,000," alisema Ndugai. "Nilipata fedha nyingi, lakini nyingi zikapotea pia baada ya kununua bidhaa kibao na kubaki nazo ndani wakati kasi ya watu kufuata kikombe ikikatika ghafla.

"Safari hii kama wageni wakija tena kwa wingi nitakuwa makini na kuzingatia ushauri wa Babu.”

Kina mama waliojitambulisha kwa majina ya Esuvati Loishiye na Anna Laizer, walisema Babu amesaidia kubadilisha hali ya Samunge kupitia tiba ya kikombe kwa sababu tangu wakati huo, hivi sasa wameamka na kuchangamkia biashara ya kupika na kuuza chakula.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post