MWENENDO wa utendaji kazi wa baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya sasa umeanza kuonyesha dalili za kukumbwa na kiwewe cha kutoteuliwa tena katika safu mpya inayotarajiwa kutangazwa wakati wowote na Rais John Magufuli.
Hali hiyo imebainika wiki iliyopita baada ya Rais Magufuli kulitaja hadharani jina la Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuwa mmoja wa watu waliojihakikishia nafasi katika Serikali yake kutokana na utendaji kazi wake.
Rais Magufuli aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wazee wa Dar es Salaam ambapo pamoja na kusifia utendaji kazi wa Makonda, alisema umma usishangae iwapo atampandisha cheo.
Makonda anatajwa kufanikiwa kwa kiwango kikubwa kuhamasisha uchangiaji wa elimu na kusimamia shughuli za maendeleo.
“Najua watu wanauliza sana ni lini nitateua wakuu wa mikoa na wilaya. Wala hawatajua, lakini ninaendelea kuwachambua, angalau mheshimiwa Makonda umeshajihakikishia angalau kupata. Lakini na wewe sasa usianze kulala,” alisema Rais Magufuli.
Kauli hiyo ya Magufuli imeonekana kuwaibua baadhi ya wakuu wa wilaya ambao kwa zaidi ya wiki moja sasa wamekuwa wakisambaza wenyewe au mawakala wao picha za utendaji kazi wao kwa jamii kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.
Picha ambazo zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii zinawaonyesha viongozi hao wakijishughulisha na kazi za kutatua migogoro ya ardhi, kupanda miti, kufanya usafi wa mazingira, kuhamasisha uchangiaji wa vifaa vya elimu na hata kushiriki shughuli za uokoaji wa majanga.
Mmoja wa viongozi hao ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela ambaye tayari picha zake zimezua mjadala mkubwa katika mitandao ya Whatsap, facebook na Jamii Forum.
Katika mitandao hiyo, picha za Kasesela zinamuonyesha akiwa anawaokoa baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mboliboli, Tarafa ya Pawaga wilayani humo ambao kijiji chao kimezingirwa na maji baada ya kukumbwa na mafuriko.
Picha iliyozua gumzo zaidi ni ile inayomuonesha Kasesela akiwa amembeba mgongoni mtu aliyedaiwa kuwa ni mpiga picha. Katika picha hiyo, maoni mbalimbali yametolewa kwenye mitandao ambako wachangiaji wengi wameeleza kuwa anafanya kazi kwa kujionyesha ili Rais Magufuli amkumbuke wakati wa uteuzi.
Mmoja wa wanasiasa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, aliweka picha hiyo katika akaunti yake ya facebook na kuandika kuwa; “Hizi ndizo siasa za Tanzania, Mkuu wa Wilaya anapombeba mpiga picha!”
Kasesela alipoulizwa na MTANZANIA Jumamosi kupitia simu yake ya kiganjani iwapo anafanya kazi ili Rais Magufuli amuone au la, kwanza alikiri kuwa picha iliyotumwa na Msigwa ni yake na kwamba tangu alipofika katika wilaya hiyo amekuwa akijishughulisha na uokoaji watu katika mafuriko hayo.
“Toka naingia niko kazini, toka nimefika ni mafuriko, mafuriko hata sasa niko huku porini nafyeka ili kutengeneza mahali pa kuwahifadhi watu waliookolewa, tuko tunafanya kazi,” alisema Kasesela.
Alisema hata picha iliyozua gumzo mtandaoni inayomuonyesha akiwa amembeba mpigapicha badala ya kuokoa watoto inatafasiriwa vibaya lakini lengo lake lilikuwa ni kumwokoa asiharibu vifaa vyake vya kufanyia kazi.
“Kuokoa watu 399 sio mchezo, yule mpiga picha kwenye ile picha iliyozua gumzo mtandaoni alikuwa ameshika chombo nami nilikuwa nimekwishavua viatu, kuna watu wanapotosha kauli ya Rais Magufuli,” alisema Kasesela.
Picha nyingine katika mitandao ya kijamii inamwonyesha Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mrisho Gambo, akila chakula na wananchi eneo ambalo linaonekana kuwa ni shamba huku nyingine ikimwonyesha akiwa amejitwisha mawe kichwani.
Alipoulizwa Gambo kupitia simu yake ya kiganjani ili kujua iwapo picha ile ni yake na kwamba alikuwa katika tukio lipi, alipokea na kusikiliza kisha akaomba apewe muda kidogo amalizane na watu aliokuwa nao.
Hata hivyo, Gambo alipotafutwa baadaye hakupokea simu.
Mwingine aliyezua gumzo ni Mkuu wa Wilaya ya Hai, Antony Mtaka ambaye picha zake katika mitandao ya kijamii zinamuonyesha akiwa amekaa chini akizungumza na wananchi ambao wamesimama.
Mtaka alipoulizwa kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu tukio hilo, aling’aka kwa ukali huku akidai kuwa waandishi wa habari wanamfuatilia na kumsakama na kwamba wengi wana chuki na Serikali.
Akizungumza kwa sauti ya ukali, ya juu huku akitamka maneno machafu ambayo hatuwezi kuyaandika gazetini, Mtaka alisema hafanyi kazi na vyombo vya habari kwa sababu hahitaji kuonekana utendaji wake na mtu yeyote na kwamba yeyote anayemuhoji kuhusu hilo ni upumbavu.
“Mimi sifanyi biashara ya kuonekana ili ifanyeje? Muulize aliyenipiga picha kuwa ilikuwa wapi, sifanyi kazi na media mimi, hatufanyi kazi ya kuonekana kwenye media, mimi upumbavu huo sifanyi,” aling’aka Mtaka.
Alipobanwa kuwa ni kwanini anaruhusu picha zake kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kama hataki kuonekana, aling’aka tena kwa ukali huku akieleza tuhuma za moja kwa moja kwa gazeti hili kuwa limefanya kazi ya kuichafua Serikali kwa muda wa miaka minane mfululizo hivyo ni ajabu sasa kuanza kuisifia Serikali ya Rais Magufuli.
“Mmefanya kazi ya kuichafua Serikali kwa miaka nane leo hii Serikali ya Magufuli imekuwa nzuri,” alihoji kwa sauti ya ukali Mtaka.
Tangu Rais Magufuli alipotangaza Baraza la Mawaziri Desemba mwaka jana, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wameripotiwa kuishi kwa hofu ya kutemwa katika uteuzi utakaofanywa.
Tayari Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amekwishawaaga baadhi ya watumishi wa umma mkoani Mwanza, hatua inayoelezwa na wachambuzi na wafuatiliaji wa siasa za hapa nyumbani kuwa inatokana na kutokuwa na uhakika wa kuteuliwa.
Na Agatha Charles-Mtanzania
Social Plugin