Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAWAZIRI MRAMBA NA YONA SASA KUTUMIKIA KIFUNGO CHA NJE KWA KUFANYA USAFI KATIKA HOSPITALI YA PALESTINA SINZA DAR ES SALAAM






Hatimaye aliyekuwa waziri wa fedha, Basil Mramba na aliyekuwa waziri wa nishati na madini Daniel Yona, wamepewa adhabu ya kifungo cha nje, ambapo watakuwa wanafanya shughuli za kijamii katika hospitali ya Palestina Sinza, Dar es Salaam ikiwemo usafi wa mazingira. 

Vigogo hao wa serikali walikuwa wanatuhumiwa kuisababishia serikali hasara ya sh. Bilioni 11.7, baada Mramba kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingereza ya ukaguzi wa madini ya dhahabu bila kupata ushauri kutoka TRA.



Mchakato huo wa vigogo hao wa serikali kupata kifungo cha nje, ulitokana na magereza kuandika barua katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambayo ilikuwa na orodha ya majina likiwemo la Mramba na Yona. 



Barua hiyo ambayo iliandikwa Desemba 5, mwaka jana na magereza ilikuwa inaeleza kuwa imeona wafungwa hao wanastahili kufanya kazi za kijamii nje na gereza. 

Magereza waliandika barua hiyo kwa kufuata sheria ya huduma kwa jamii namba 6 ya mwaka 2002 kifungu cha tatu kinaeleza kuwa mtu yeyote anapokuwa ametiwa hatiani kifungo kisichozidi miaka mitatu na faini kina ruhusu mfungwa kupewa adhabu ya kifungo cha nje. 



Baada ya hakimu mkuu mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha kupata barua hiyo alitoa amri kwa maofisa wa ustawi wa jamii kwenda gerezani kuchunguza kama kweli walichokidai magereza ni cha kweli. 



Vigogo hao watatakiwa kufika katika hospitali hiyo saa moja asubuhi kuanzia jumatatu hadi ijumaa, ambapo watatakiwa kufanya shughuli hizo kwa saa nne kila siku. 



Kama magereza wasingewaona Mramba na Yona kuwa wanaweza kutumikia adhabu ya kifungo cha nje walitakiwa kumaliza kifungo chao cha miaka miwili jela Novemba 5, mwaka huu. 



Julai 6, mwaka jana, mahakama ya Kisutu iliwahukumu kwenda jela miaka mitatu Mramba na Yona baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7.
Via>>ITV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com