Baada ya kiwango chake kushuka ghafla na kutokuwa na uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza cha Simba, kiungo Mwinyi Kazimoto ameanza mazoezi ya kubadilisha fani, huku umri ukionekana kumtupa mkono.
Kiungo huyo ambaye miaka miwili aliyoichezea Markhiya ya Qatar haikuwa na mafanikio aligeuka bondia baada ya kumvamia na kumjeruhi kwa kipigo cha ngumi, mateke, makofi mwandishi wa gazeti la Mwananchi aliyefika mkoani Shinyanga kuandika habari, Mwanahiba Richard.
Mwinyi anayedai kuwa na umri wa miaka 27, alifanya kitendo hicho jana, mjini Shinyanga.
Kazimoto alifanya kitendo hicho kinachoonyesha wazi kuwa, soka sasa limemshinda na kuutamani ubondia, baada ya mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Kambarage akimtuhumu Mwanahiba kumuandika vibaya katikati ya mwaka jana.
Kiungo huyo aliyewahi kuichezea JKT Ruvu kabla ya kutimkia Msimbazi, alimvamia Mwanahiba na kumjeruhi mwilini katika mazoezi ya asubuhi, huku akiwa hana ushahidi wa anachokilalamikia, zaidi ya kudai aliambiwa na washikaji zake.
“Alinivamia baada ya mazoezi ya timu yao na kunihoji kwa nini nilimwandika vibaya mwaka jana, nilimhoji ana hakika na anachokisema na kudai aliambiwa tu na washikaji zake kuonyesha anafanya mambo kwa kubahatisha,” alisema Mwanahiba akiwa Hospitali ya Shinyanga kwa ajili ya matitabu.
Mwanahiba alisema siku za nyuma Kazimoto alishawahi kumpigia simu kadhaa akimtusi na akamtisha kwa kumpa siku saba ili ataje mtu aliyempa habari aliyoiandika mwaka jana baada ya Simba kucharazwa bao 1-0 na Prisons Mbeya.
“Ndipo leo (jana) baada ya mazoezi akanivamia na kunipiga ngumi na makofi, huku akitamba kuwa niende kokote na yeye hajali, kauli ambazo hata kocha wake, Jackson Mayanja na nahodha Mussa Hassan Mgosi waliisikia, kuonyesha alikusudia,” alisema.
Mwanahiba alisema tukio hilo ameliripoti Kituo cha Polisi cha mjini Shinyanga kwa kufunguliwa jalada lenye namba SHY/RB/895/2016, kisha kupelekwa hospitali kwa matibabu, huku Kazimoto akifuatwa katika kambi ya timu hiyo, iliyopo Virgimark Hotel.
Social Plugin