Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Ernest Mangu kufuatia vifo vya askari watatu waliopoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea jana tarehe 06 Februari, 2016 katika kijiji cha Isuna, Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida.
Askari waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Inspekta Miraji Mwegelo, Sajenti Elias Mrope na Sajenti Gerald Ntondo.
Katika salamu hizo Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na vifo vya askari hao, ambao wamekutwa na mauti wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kikazi.
"Kupitia kwako Mkuu wa Jeshi la Polisi natoa pole nyingi kwa familia za Askari waliopoteza maisha, Ndugu, Jamaa na Marafiki pamoja na askari wote wa Jeshi la Polisi Tanzania ambao wameguswa kwa namna ya pekee na msiba huu" Amesema Rais Magufuli.
Ameongeza kuwa anaungana na wote walioguswa na vifo hivyo katika kipindi hiki kigumu, na amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Rais Magufuli pia amewatumia salamu za pole Askari walioumia katika ajali hiyo, akiwemo Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani katika Mkoa wa Singida Mrakibu wa Polisi Peter Magira na kuwaombea wapone haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kila siku.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
07 Februari, 2016
Social Plugin