Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SABABU ZA TCU KUFUTA USAJILI WA VYUO VIWILI TANZANIA



Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya


Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imevifutia usajili vyuo vikuu viwili vya Mtakatifu Yosefu (SJUIT) kampasi ya Songea mkoani Ruvuma kwa kutoa elimu isiyokuwa na viwango bora kwa wanafunzi.

Zaidi ya wanafunzi 2,000 wanatarajiwa kuhamishiwa kwenye vyuo vingine vinavyofundisha masomo waliyokuwa wanayasoma chuoni hapo.

Vyuo vilivyofutiwa usajili ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za Kilimo na Teknolojia (SJUCAST) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Teknolojia ya Habari (SJUCIT).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya, alisema tume imejiridhisha kuwa vyuo hivyo viwili havitoi elimu inayostahili kwa viwango vinavyotakiwa vya vyuo vikuu.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu, TCU ina mamlaka ya kusimamia na kudhibiti ubora na usimamizi wa uendeshaji wa vyuo vikuu vya nchini.

“Kwa muda mrefu katika vyuo vikuu vya sayansi za kilimo, teknolojia na teknolojia ya habari kumekuwa na mlolongo wa matatizo mengi kama ya ubora, uongozi, ukiukwaji wa sheria na taratibu za uendeshaji wa chuo kikuu kama zilivyobainishwa na sheria,” alisema Profesa Mgaya.

Profesa Mgaya alisema TCU ilifanya jitihada kukitaka SJUIT kuhakikisha vyuo vikuu vishiriki vyake vinatoa elimu inayokidhi viwango vya ubora vilivyowekwa na Tume, lakini maelekezo yao hayakupewa uzito stahiki na uongozi wa chuo.

“Matokeo yake wanafunzi wa SJUCAST na SJUCIT wamekuwa hawapati elimu kwa viwango stahiki… Hivi sasa katika vyuo hivyo vishiriki kuna jumla ya wanafunzi 2,046 wanasoma programu za shahada na wanafunzi hao ndio waathiriki wakuu wa matatizo kwenye vyuo hivyo vishiriki,” alisema.

Profesa Mgaya alisema wanafunzi hao watahamishiwa kwenye vyuo vingine kwa gharama za Chuo Kikuu cha SJUIT, na kwamba wanafunzi wote wametakiwa kuondoka chuoni hapo mara moja baada ya kukamilisha taratibu za kukabidhi mali na vifaa vingine vya chuo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Aidha, alisema wanafunzi wote wanatakiwa kuripoti kwenye vyuo watakavyopangiwa wakati wa kufunguliwa kwa muhula wa pili na vyuo watakavyowapangia vitatangazwa kupitia tovuti ya TCU.

Alisema wanafunzi waliokuwa wanasoma Shahada ya Sayansi za Kilimo na Uhandisi watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Sikoine cha Kilimo (SUA) na Shahada ya ualimu wa sayansi watahamishiwa katika mojawapo ya vyuo vikuu cha SUA, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).

Aliendelea kufafanua kuwa wanafunzi ambao wanasoma Shahada ya Ualimu na Sayansi ya Kompyuta watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (RUCU).

Profesa Mgaya alisema wanafunzi wote ambao wanasoma Shahada na Stashahada ya sayansi na kompyuta watahamishiwa Chuo Kikuu cha Sokoine.

Aidha, alisema wanafunzo wote waliohamishwa ambao hawajakamilisha mitihani yao ya mwisho wa muhula wa kwanza au hawakufanya mtihani watatakiwa kufanya mitihani hiyo katika vyuo vikuu watakavyohamishiwa kwa utaratibu maalum utakaoandaliwa na chuo husika.

Profesa Mgaya alisema wanafunzi wote ambao ni wanufaika wa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, mikopo yao itapelekwa katika vyuo walivyohamishiwa.

Profesa Mgaya alivitaka vyuo vikuu nchini kuhakikisha vinazingatia utoaji wa elimu inayokidhi viwango vya ubora vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.

Alisema hawatasita kuchukua hatua kwa chuo kikuu chochote kitakachobainika kutoa elimu isiyokidhi viwango vya ubora kwa kisingizio cha aina yoyote..


CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com