Watu sita wanaodaiwa kuwa majangili, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuitungua helikopta ya doria na kusababisha kifo cha rubani wake katika pori la akiba la Maswa.
Kukamatwa kwa watu hao kumekuja siku moja baada ya Rais, John Magufuli, kutoa agizo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuwakamatwa waliohusika na tukio hilo na kufikishwa katika mkono ya sheria.
Kauli hiyo ya Rais iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli mbali na kusikitishwa na tukio hilo, pia aliuakikisha umma kuwa serikali itahakikisha inaendeleza mapambano dhidi ya ujangili kwa nguvu zote na kuwataka wananchi na wadau mbalimbali wa hifadhi ya wanyamapori kutokatishwa tama.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Gemini Mushy, jana alithibitisha kukamatwa kwa watu hao.
Alisema awali walikamata watu wawili, juzi watatu na jana mmoja wote wakiwa wakazi wa Simiyu na uchunguzi bado unaendelea.
Ijumaa iliyopita, watu wasiojulikana, waliitungua helikopta hiyo wakati ikifanya doria katika pori hilo baada ya kuwapo taarifa kwamba majangili walikuwa wameua tembo mmoja.
Katika tukio hilo, rubani wa helikopta hiyo raia wa Uingereza, Rodgers Gower (37) alikufa, huku mwenzake Nicky Bester wa Afrika Kusini akinusurika.
Social Plugin