Wabunge wa upinzani, wakiwamo wanaootoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamepata pigo la aina yake baada ya jukumu mojawapo muhimu la kamati wanayopaswa kuiongoza kuondolewa kwao, imefahamika.
Kamati hiyo ni ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) ambayo imehamishiwa kwenye kamati mpya inayoongozwa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika kufuatilia yanayoendelea kwenye vikao vya Bunge la 11 mjini hapa mwishoni mwa wiki, Nipashe imebaini kuwa majukumu hayo muhimu yaliyohamishwa PAC ni yale yanayohusiana na hesabu za mashirika ya umma. Majukumu hayo sasa yamehamishiwa kwenye kamati mpya ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Jimbo la Sumve (CCM), Richard Ndasa, huku makamu mwenyekiti akiwa Lolesia Bukwimba (Busanda-CCM).
Naibu Katibu wa Bunge anayeshughulikia masuala ya Bunge, John Joel, aliithibitishia Nipashe juu ya kuwapo kwa mabadiliko hayo, akisema kwamba ni kweli PIC imepewa jukumu la kusimamia hesabu za mashirika ya umma kutokana na kanuni za Bunge, toleo la Januari 2016.
Alisema uamuzi wa kupeleka jukumu hilo PIC, umetokana na pendekezo la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kutokana na PAC iliyopita kushindwa kutimiza majukumu yake iliyopewa.
“Ni kweli, kabla hujaniuliza fanya utafiti ujue ni kitu gani kilikuwa kinaendelea zamani. Ujue ni kwa nini PAC ilipewa hilo jukumu halafu uniambie PAC walitekeleza hilo jukumu walilopewa? Kuna majukumu walipewa na hawakutimiza,” alisema Joel.
Alipoulizwa majukumu ambayo kamati iliyopita haikuyatimiza, Joel alisema: “Ni hayo hayo ya kukagua mashirika na ndiyo maana CAG akashauri ianzishwe kamati nyingine.”
Kambi ya upinzani bungeni inaundwa na wabunge wengi wanaotoka vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.
Katika mabunge yaliyotangulia, hesabu za mashirika ya umma zilikuwa zikisimamiwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia (Chadema), Zitto Kabwe. Hivi sasa, Zitto ni Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia ACT-Wazalendo.
Kamati hiyo pia iliwahi kuongozwa na asliyekuwa Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mara zote PAC ndiyo iliyokuwa mstari wa mbele katika kuibua ‘madudu’ mbalimbali yanayohusiana na rushwa na ufisadi bungeni na kuilazimu serikali kubadili mawaziri wake mara kadhaa.
Baadhi ya mambo yaliyowahi kuibuliwa na PAC ni pamoja na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo ripoti yake ilisababisha mawaziri wawili wa serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete na maofisa wengine kadhaa wa juu kuachia ngazi. Taarifa ya PAC kuhusiana na ripoti ya CAG mwaka 2012 pia ilisababisha vigogo kadhaa, wakiwamo mawaziri, kung’olewa.
Kadhalika, nguvu za PAC chini ya upinzani ziliwahi kudhihirishwa na mwenyekiti wake wakati alipoamuru kuwekwa mbaroni kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji baada ya kukataa kuipa kamati hiyo mikataba ya gesi na mafuta.
Hivi sasa, PAC ambayo inaelezwa kuwa haitakuwa tena na jukumu la kushughulikia hesabu za serikali na mashirika ya umma, inaongozwa na Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilal (CCM), anayeshikilia nafasi ya makamu mwenyekiti. Yeye (Hilal) anasubiri kukamilika kwa maridhiano juu ya kupanga wajumbe wa kamati hiyo kati ya kambi ya upinzani bungeni na ofisi ya Spika ili wachague mwenyekiti ambaye anatakiwa awe miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo wanaotoka katika kambi ya upinzani.
Taarifa zaidi ambazo Nipashe imezipata zinaeleza kuwa kambi ya upinzani imepanga kumpeleka kiongozi wake, Freeman Mbowe, kuwa Mwenyekiti wa PAC huku Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), akitarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Baadhi ya wajumbe wa PAC wanaotoka CCM waliozungumza na Nipashe kwa sharti la kutotajwa majina walikiri kuwa kitendo cha hesabu za masharika ya umma kuondolewa kwenye kamati hiyo ni mwendelezo wa vitendo vya kulinyima Bunge nguvu.
“Kimsingi kamati za kusimamia fedha za umma ni mbili na zinatakiwa ziwe chini ya kamati ambayo inaongozwa na kambi ya upinzani.
Kamati hizo kwa sasa ni LAAC na PAC. Sasa walichofanya ni kuondoa mashrika ya umma huku na kuyapeleka PIC. Kimsingi inatakiwa sasa na hiyo kamati (PIC) iwe chini ya mwenyekiti wa upinzani,” alisema mmoja wa wajumbe hao wa PAC na kuongeza:
“Vinginevyo tutakuwa tunafifisha mamlaka ya Bunge. Ukiangalia huu ni mwendelezo wa kulibana Bunge na kulifanya kibogoyo, kama ambavyo walianza kusema majadiliano yasirushwe moja kwa moja na TBC (Shirika la Utangazaji Tanzania), halafu ukiuliza kila kitu wanasema ni agizo la Rais, sasa sijui ni kweli au wanampakazia.”
Awali, baada ya kamati za Bunge kutangazwa, kambi ya upinzani ilisusia uchaguzi wa wenyeviti kwa madai kuwa maombi ya wabunge wao walioomba kupangwa kwenye kamati nyeti za kusimamia serikali zikiwamo PAC na LAAC, hayakuzingatiwa.
Mbunge mwingine wa PAC alisema kwa kuondolewa jukumu la kusimamia hesabu za mashirika ya umma, PAC imepunguziwa nguvu na suala hilo litawaletea shida baadaye kwa sababu kikanuni na desturi ya mabunge ya nchi za Jumuiya ya Madola, kamati zinazoisimamia serikali hasa kwenye mambo ya fedha huwa zinatakiwa ziongozwe na wabunge wa kambi ya upinzani.
ZITTO AFUNGUKA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa PAC kwenye Bunge la 10, Zitto, alisema si kweli kwamba kuna jukumu walilopewa na kushindwa kulitimiza.
“Kwa kweli tulitimiza majukumu yetu yote. Na ili tufanye kazi yetu kwa ufanisi, tuliigawa kamati, eneo moja likawa chini ya Makamu Mwenyekiti (Deo Filikunjombe) na moja chini yangu. Deo mashirika na mimi serikali.
Hata hivyo, kazi ilikuwa kubwa na muhimu kugawa PAC kuwa na PIAC na PAC. Isipokuwa, PIC ya sasa haina mamlaka ya kushughulikia hesabu za mashirika ya umma kwa mujibu wa kanuni. Kamati za mahesabu ni mbili tu, PAC na LAAC,” alisema Zitto.
Aliongeza kuwa iwapo Bunge linataka PIC ishughulike na hesabu za mashirika ya umma, itabidi iitwe Public Investments Account Committee (PIAC) na itabidi iongozwe na mbunge wa upinzani na siyo wa CCM.
“Kanuni za Bunge za sasa hazielekezi PIC kushughulikia taarifa ya CAG kuhusu mahesabu ya mashirika ya umma. Pia kanuni haziipi PAC mamlaka hayo pia. Kikanuni, hivi sasa mahesabu ya mashirika ya umma hayana kamati,” alisema Zitto.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mbowe, hakuwa na nafasi nzuri ya kuzungumzia suala hilo kwani alipogiwa, alipokea simu yake na kusema hayupo eneo zuri anatoka kanisani na akiwa vizuri atazungumza.
KANUNI ZA BUNGE 2016 ZINASEMAJE?
Kwa mujibu wa Kanuni za kudumu za Bunge, toleo la Januri 2016, nyongeza ya nane sehemu ya nne, inasema kanuni za kudumu za Bunge zinazosimamia matumizi ya fedha za umma zitakuwa ni PAC na LAAC.
Sehemu ya nne, (14) (a) inaeleza majukumu ya PAC kuwa ni “kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika wizara za serikali, yaliyoainishwa katika taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.”
Kadhalika, sehemu ya 14(b) inaeleza majukumu ya PAC kuwa ni kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yaliyokwishatolewa na kamati hiyo yenye lengo la kuondoa matatizo hayo; na 14(c) inaelekeza jukumu la kutoa mapendekezo na ushauri kwa wizara za serikali kuhusu matumizi mazuri ya fedha za umma ili kupunguza matumizi mabaya ya fedha za umma.
Katika eneo hilo la nyongeza ya nane sehemu ya tatu (12), inataja majukumu zaidi ya PIC kuwa ni (a) kuchambua na kubaini iwapo utekelezaji wa miradi ya uwekezaji wa umma una ufanisi na kuwa umezingatia taratibu na sheria na miongozo mujarabu ya biashara; na
(b) kuchambua na kujadili taarifa ya mwaka ya msajili wa hazina na Mashirika ya Umma na kampuni ambazo serikali ina hisa.
CHANZO: NIPASHE
Social Plugin