Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), umesema ndoa zinazofungishwa na viongozi wa dini ambao hawana leseni au leseni zao zimeisha muda wake hazitambuliwi na serikali.
Aidha, Rita imesema viongozi wa dini ambao watafungisha ndoa bila leseni au wakiwa na leseni ambazo muda wake umekwisha watapelekwa kwenye bodi ya muunganisho wa wadhamini; ambako hatua zaidi huchukuliwa dhidi yao.
Katika hali inayoonyesha kuwa kuna ndoa nyingi batili zinazofungwa hata kwenye nyumba za ibada, Rita ilitoa tangazo katikati ya wiki ikitaka wale wote wanaofungisha ndoa kwenye madhehebu kuwa na leseni zilizo hai.
Tangazo hilo lilitolewa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Rita, ambaye pia ni Msajili Mkuu wa Ndoa na Talaka.
Rita ilitaka viongozi wa madhehebu hayo ya dini wasajiliwe na kuwa na leseni iliyo hai ambayo hutolewa na RITA.
Msemaji wa RITA, Jafari Malema, alisema viongozi wa dini ambao hawatatekeleza agizo hilo, mamlaka zao zitachukuliwa hatua.
“Mfano kama ni dhehebu la Roman tunajua wapi tuandike barua na kuipelekea na kwa Waislam nao tunawaandikia barua ili kuwakumbusha kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni zilizopo ili mambo yasifanyike kiholela,” alisema.
Alisema RITA haitawapeleka mahakamani viongozi wa dini watakaokiuka sheria bali wataitwa kwenye bodi na kuongeza kuwa ndoa ambazo zitafungishwa na viongozi hao wasio na leseni, hazitatambuliwa kiserikali.
“Kiongozi wa dini akifungisha ndoa bila kuwa na leseni kwa imani ya dini husika ndoa hiyo itakuwa halali, lakini kwa upande wa serikali haitakuwa halali kwa sababu mtu aliyefungisha ndoa hajafuata taratibu na sheria za nchi,” alisema.
Aidha, alisema kati ya viongozi hao wapo ambao leseni zao zimeisha na wengine hawajawahi kujisajili kabisa.
Tangazo hilo lilisema kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 2002 sura ya 29, ni lazima viongozi hao wawe wamesajiliwa na kuwa na leseni iliyo hai inayotoka kwa wakala.
Rita iliwakumbusha viongozi hao kujisajili ili wapate leseni za kufungisha ndoa na kwa wale ambao zimeisha muda wake wazihuishe ili waweze kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria.
Pia Rita iliwakumbusha viongozi hao kuwa kufungisha ndoa bila ya leseni ni kosa kisheria na kwamba RITA haitasita kuchukua hatua.
Chanzo-Nipashe
Social Plugin