Jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara limethibitisha kupokea maiti nne za wafanyabiashara wa kitanzania waliouwa na majambazi nchini Msumbiji na kuporwa mali na fedha katika kijiji cha Mtoro wilaya ya Mtepwezi jimbo la Deboderobage.
Akithibitisha kupokelewa kwa maiti hizo kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara Henrry Mwaibambe amesema watanzania hao walikuwa ni wafanyabiashara ya dhahabu na wamepigwa risasi wakiwa eneo la machimbo ya dhahabu.
Amesema baada ya uchunguzi wa maiti hizo kufanyika katika hospitali ya mkoa wa Ligula imethibitisha watanzania hao wameuawa kwa kupigwa risasi na vitu vyenye ncha kali.
Hata hivyo daktari mfawidhi wa hospitali ya Ligula Diksoni Saini hakutaka kuonyesha ushirikiano kwa waandishi na kudai hana taarifa za kupokelewa kwa maiti nne katika hospitali ya mkoa ya Ligula.
Maiti hizo zimepokelewa mkoani Mtwara na baada ya kukabidhiwa ndugu wa marehemu zilipelekwa katika msikiti wa Majengo kwa ajili ya kufanyiwa usafi na kusafirishwa kwa gari kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazishi.
Via>>ITV
Social Plugin