Waziri mkuu Mh Kassim Majaliwa amemtaka mtendaji mkuu wa wakala wa vipimo Tanzania kumpa maelezo kwa maandishi ya sababu za kuzuia utumiwaji wa mita za kupima kiwango cha mafuta kinachopakuliwa bandarini kutoka melini (flow meter) kwa kipindi cha miaka mitano jambo lililosababisha serikali kupata hasara ya mamilioni ya shilingi huku mita hizo zikianza kufanya kazi siku moja tu kabla ya kufanya ziara hiyo bandarini hapo.
Waziri mkuu Mh. Kassim Majaliwa ameifanya ziara hiyo ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam ili kujionea namna shughuli za upakuaji wa mafuta kutoka melini zinavyofanyika bila ya uwepo wa mwanya wa ukwepaji wa kodi kwa kutembelea maeneo yenye mita za kupimia mafuta hayo yaani flow meters na kubaini kuwa mita hizo licha ya kununuliwa kwa fedha nyingi hazijafanya kazi kwa kipindi cha miaka mitano baada ya uwepo wa zuio kutoka kwa wakala wa vipimo Tanzania na kuanza kufanya kazi siku moja kabla ya ziara hiyo ya waziri mkuu na kutaka maelezo.
Mtendaji mkuu wa wakala wa vipimo nchini Magdalena Chuwa nae akapata fursa ya kutoa maelezo ya sababu za kuzuia kutumika kwa mita hizo jambo lililoisababishia serikali hasara.
Mara baada ya maelezo hayo waziri mkuu Kassim Majaliwa anatoa maagizo kadhaa mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali bandarini hapo ambapo kwanza anamwagiza mtendaji mkuu wa wakala wa vipimo nchini kumwandikia barua yenye maelezo ya sababu za kuzuia utumiwaji wa mita hizo.
Pia waziri mkuu anatoa muda wa mwezi mmoja kung`olewa kwa mabomba yote ya mafuta yaliyounganishwa bila idhini ya mamlaka ya bandari nchini jambo linalotoa mwanya wa uwepo wa wizi wa mafuta kutokana na kukosekana kwa ufuatiliaji.
Aidha waziri mkuu anamuagiza msajili wa hazina kwa kushirikiana na mwanasheria mkuu kuangalia namna ya kuvunja mkataba na kampuni ya Oryx Energys inayomiliki matanki ya kuhifadhia mafuta kwa asilimia 50 kwa 50 na serikali.
Waziri mkuu huyo anataka uwepo wa mfumo maalum utakaodhibiti mianya ya upitishwaji wa mafuta katika bandari ya Dar es Salaam bila ya ukwepaji wa kodi ili kuliwezesha taifa kukusanya mapato ya kutosha kutoka bandarini kabla ya serikali kuanza kujielekeza katika kuimarisha sekta ya reli nchini.
Social Plugin