Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU MSTAAFU FREDRICK SUMAYE AMSUBIRI DC MAKONDA MABWEPANDE

 
Waziri Mkuu mstafu, Fredrick Sumaye, hajachukua uamuzi mpya wa kuondoa wavamizi kwenye shamba lake lililopo Mji Mpya, Mabwepande, Dar es Salaam licha ya muda wa suluhu kuwa ulishamalizika.

Sumaye amesema mustakabali wa shamba hilo ameuacha mikononi mwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.

Akizungumza na Nipashe jana, Sumaye alisema ingawa siku 14 zilizoombwa na Makonda kwa ajili ya kutafuta hatma ya shamba hilio zimeisha, hajachukua uamuzi wowote kuhusu suala hilo kwa sasa kwa sababu Makonda alishaahidi kulitafutia ufumbuzi.

“Ndugu yangu mimi nafahamu muda alioutoa DC Makonda umeisha ila sina maamuzi yoyote kwa sasa, nilituma watu wangu kwenda kuonana naye lakini hadi leo hii hajatujibu,” alisema Sumaye ambaye aliweka rekodi ya kuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo.
“Bado tunasubiri.”

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Makonda aliitisha mkutano wa wakazi wa Mji Mpya, Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na wamiliki wa mashamba na viwanja wa eneo hilo.

Sumaye aliutumia mkutano huo kuonyesha wavamizi zaidi ya 100 hati za umiliki za ardhi hiyo yenye ukubwa wa heka 33.

Katika mkutano huo, Makonda aliomba apewe wiki mbili ili kutatua mgogoro huo ikiwa ni pamoja na kupitia sheria za umiliki wa ardhi hiyo kama zilikiukwa na Sumaye au la.

Sumaye alikuwa Waziri Mkuu katika muda wote wa serikali ya Rais wa tatu, Benjamin Mkapa, kati ya 1995-2005.

Aidha, Makonda aliwaeleza wavamizi hao kuwa endapo Sumaye atashinda kwenye shauri hilo, Waziri Mkuu wa zamani huyo ndiye ataangalia namna ya kuwasaidia eneo la kuishi kadri atakavyoona inafaa.

Katika utetezi wake siku hiyo, Sumaye alisema baada ya serikali kubadili matumizi ya ardhi, aliacha kulima miaka mitatu iliyopita ili ajenge Chuo Kikuu.

Uvamizi kwenye shamba hilo ulitokea mwishoni mwa mwaka jana ambapo zaidi ya watu 100 waligawana maeneo kwenye shamba hilo.
Kati yao, baadhi wameshajenga nyumba za kuishi za matofali.
Na Romana Mallya-Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com