Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.
Ikiwa zimepita siku 40 tangu aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, kusema baadhi ya wafanyabiashara waliounga mkono upinzani wanasumbuliwa kwenye kodi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amemjibu bila kumtaja jina moja kwa moja.
Januari Mosi, mwaka huu, akitoa salamu za mwaka mpya katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Monduli, Lowassa alisema amepokea malalamiko ya kuwapo kwa uonevu na vitisho kwa wadau walioonekana kuunga mkono vyama vya upinzani wakati wa kampeni.
Alisema hali hiyo ilitokea ilhali hatua ya wafanyabiashara hao haikukiuka Katiba, hivyo kuzitaka idara zinazohusika kuchukua hatua ili kuepusha matatizo yasiyo ya lazima.
“Imeanza kutokea tabia ya kuwalaumu na 'kuwa-harass' (kuwasumbua) wale waliounga mkono vyama vya upinzani. Wanawa-harass kwenye kodi, nasikia wanawa-harass kwenye miradi na hata mitaani, hili si jambo zuri,” alisema Lowassa.
DK. MPANGO AMJIBU
Jana, Dk. Mpango akizungumza na wafanyabiashara kwa lengo la kufahamiana na kuelezana mikakati ya serikali, alisema operesheni iliyoendeshwa bandarini kwa wafanyabiashara waliokwepa kulipa kodi, haikuwa na lengo la kuwabana wale waliosaidia upinzani wakati wa uchaguzi mkuu.
Alisema hatua ya serikali ya kukusanya kodi kwa nguvu kwa wafanyabiashara hao haikuwa na lengo la kuwanyanyasa.
“Dhana iliyopo sasa kuwa hatua iliyochukuliwa na serikali bandarini ya makontena kuwa iliwalenga baadhi ya wafanyabiashara waliousaidia upinzani, si ya kweli,” alisema.
Kauli hii ya Dk. Mpango inatafsiriwa ilikuwa ikimjibu Lowassa kwa kuwa tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu ni kiongozi huyo pekee aliyekuwa akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ndiye alijitokeza hadharani na kulalamikia kunyanyaswa kwa wafanyabiashara waliokuwa wakiunga mkono upinzani wakati wa kampeni.
Akizungumza na wafanyabiashara hao jana, Dk. Mpango alisema serikali ya awamu ya tano inatambua mchango wa wafanyabiashara hivyo itashirikiana nao katika kujenga uchumi wa nchi.
Alisema dhana kuwa hatua iliyochukuliwa na serikali bandarini iliwalenga wafanyabiashara waliowasaidia wapinzani wakati wa kampeni si ya kweli.
“Serikali ya Rais Dk. John Magufuli inatambua umuhimu wa uwekezaji katika uchumi wa nchi. Dhamira yangu ni kufanya kazi na wafanyabaishara wakubwa na wadogo,” alisema Dk. Mpango.
Alisema serikali ya Rais Magufuli haitawavumilia wafanyabiashara wachache ambao wanakwepa kodi na kuwataka waache tabia hiyo mara moja kwa kuwa itatumika sheria na hakuna mfanyabishara yeyote atakayeonewa.
Alisema kama kutakuwa na mfanyabishara atakayeonewa na mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), atoe taarifa wizarani haraka.
Aliongeza kuwa hapendi kuwa waziri ombaomba kwa kuwa amechoka kuwasindikiza wengine na kusema masharti ya kuomba misada ni makubwa na mengine hayatekelezeki, akitolea mfano wa kukubali sheria ya ndoa ya jinsia moja.
Alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwahudumia wanachi kwa kuwapa huduma bora za kijamii pamoja na kuwa na uchumi imara, kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kukusanya mapato.
Katika hatua nyingine, Dk. Mpango aliwaambia wafanyabiashara hao katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17, serikali itafuta ushuru na tozo ndogo ndogo ambazo zimekuwa kero kwa wafanyabiashara.
Kadhalika, alisema bajeti hiyo itajielekeza katika kujenga uchumi imara wenye viwanda, miradi mikubwa itakayoleta matokeo makubwa na ajira nyingi pamoja na maeneo wezeshi kwa ajili ya kujenga viwanda kama vile uwapo wa umeme wa uhakika, bandari na ardhi.
Dk. Mpango alisema serikali imeziagiza taasisi zake zinazojihusisha na tozo kuorodhesha na kuleta aina zote za tozo ambazo wanatoza ili kuzifuta.
Alisema serikali ya awamu ya tano inatambua umuhimu wa uwekezaji katika uchumi, hivyo itashirikiana na wafanyabiashara wakubwa na wadogo.
Waziri huyo alisema katika bajeti ijayo serikali itajielekeza katika viwanda ambavyo malighafi zake zinapatikana nchini kama vile misitu, uvuvi, madini na kilimo.
Dk. Mpango alisema kutajengwa viwanda vikubwa vitakavyoweza kuajiri idadi kubwa ya watu kama vile kiwanda cha nguo, viatu na mafuta ya kupikia.
Alisema kwa sasa msajili wa hazina ameshaelekezwa na ameanza kufanya uchambuzi kwa viwanda vilivyobinafsishwa lakini havifanyi kazi inavyotakiwa.
Dk. Mpango alisema serikali itawanyang’anya wamiliki wa viwanda hivyo na kuwapatia wabia ambao wanaweza kuviendeleza.
Alisema bajeti ijayo pia itajielekeza katika ujenzi wa reli ya kati ya kisasa ambayo inahitaji Sh. trilioni nane hadi tisa kukamilisha ujenzi wake, na serikali haiwezi kujenga kwa fedha za bajeti.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri na Sera kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Felix Mosha, alisema serikali inapaswa kutafuta mfumo ambao utalinda viwanda vya ndani, pamoja na utaratibu wa kuwekeza katika kilimo.
Alisema hakuna taifa litakalokuwa kiuchumi bila ya kuwekeza katika kilimo.
Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Stephen Ngatunga, alisema tozo nyingi ambazo wafanyabishara wanatozwa, hazina umuhimu wowote.
Alisema bandarini kuna majangili wengi wa ushuru na kodi, huku akipendekeza malipo yote kulipwa kwa shilingi badala ya dola na kuongeza kuwa TRA inapaswa kukusanya tozo ya kuhifadhi mizigo bandarini badala ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari.
CHANZO: NIPASHE
Social Plugin