AGPAHI YAPONGEZWA KWA MAPAMBANO DHIDI YA VVU NA UKIMWI MKOANI SHINYANGA

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI katika mkoa wa Shinyanga,Simiyu na Geita, Dr. Sekela Mwakyusa akitoa mada kuhusu huduma zinazotolewa na shirika la AGPAHI katika mkoa wa Shinyanga. Mada hiyo ilitolewa wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga chenye lengo la kutoa ushauri utakaomsaidia mkuu wa mkoa kutoa miongozo ya maelekezo ya utekelezaji wa shughuli za serikali katika mkoa.


Kikao hicho kimefanyika wiki iliyopita na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa, taasisi za umma na binafsi, viongozi na watendaji wa mashirika likiwemo shirika la AGPAHI lililoalikwa kwa ajili ya kuelezea huduma zinazotolewa na shirika hilo hususani katika eneo la huduma za VVU na UKIMWI kwa watoto chini ya miaka mitano.

Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga akiwemo mkuu wa mkoa huo Mheshimiwa Anne Kilango Malecela walilipongeza shirika hilo kwa jitihada linazofanya katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.

Katika kikao hicho cha ushauri wa mkoa, Dr.Mwakyusa alisema shirika lake limekuwa likifanya shughuli zake kwa ukaribu zaidi na halmashauri za wilaya za mkoa wa Shinyanga katika kutoa elimu juu ya VVU na UKIMWI kwa watu wanaoishi na VVU huku wakiwajengea uwezo watoa huduma ya elimu ya VVU na UKIMWI ngazi ya jamii wakiwemo watu wanaoshi na VVU wanaotoa huduma katika vituo vya tiba na matunzo (WAVIU Washauri). Alisema pia wanaendelea kuhamasisha uundwaji wa vikundi vya akina mama,watoto na vijana katika vituo vya tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU.

Dr. Mwakyusa aliongeza kuwa shirika lake linafanya jitihada kubwa katika kupambana na maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.Pia shirika hilo linaendelea kutoa huduma ya vipimo vya saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama katika vituo mbalimbali vya afya mkoani Shinyanga.

Kulia ni katibu tawala msaidizi mipango na uratibu mkoa wa Shinyanga George Andrea,akimsikiliza Dr. Mwakyusa. Katika kufikisha elimu ya VVU na UKIMWI kwa jamii, Dr. Mwakyusa alisema pia wamekuwa wakiendesha vipindi mbalimbali vya afya katika vyombo vya habari ikiwemo Radio Free Africa na Radio Kahama.

Dr. Mwakyusa aliongeza kuwa shirika lake mkoani Shinyanga limekuwa likijitahidi kuboresha mfumo wa afya kwa kutoa elimu na mafunzo kwa watoa huduma katika vituo vya afya, kuboresha miundo mbinu katika vituo vya afya, kutoa dawa na vifaa tiba mbalimbali vya maabara lakini pia kutoa magari kwa halmashauri na baiskeli kwa watoa huduma ngazi ya jamii ambao wanafanya kazi katika vituo vya tiba na matunzo.

Aliyesimama ni katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Abdul Dachi akiwakaribisha wajumbe wa kamati ya ushauri ya mkoa wa Shinyanga kuchangia mada zilizowasilishwa na mashirika na taasisi mbalimbali ikiwemo shirika la AGPAHI.Kulia ni mstahiki meya wa manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam,kushoto ni mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Anne Kilango Malecela.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu Mheshimiwa Hawa Ng'humbi akichangia mada iliyowasilishwa na mkurugenzi wa shirika la AGPAHI Dr. Sekela Mwanyusa. Mkuu huyo wa wilaya alipongeza shirika hilo kwa kuwahudumia wananchi wa Shinyanga ikiwemo wilaya yake kwani wamekuwa msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Anne Kilango Malecela akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Shinyanga.Mheshimiwa Anne Kilango Malecela mbali na kupongeza shirika la AGPAHI katika jitihada za kupambana VVU na UKIMWI mkoani humo akitolea mfano huduma za VVU na UKIMWI kwa watoto chini ya miaka mitano, alilitaka shirika hilo kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na sekretariati ya mkoa wa Shinyanga katika kupiga vita maambukizi ya VVU.

Mkuu wa mkoa pia alitumia fursa hiyo kuwataka wakazi wa Shinyanga kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa UKIMWI kutokana na kile alichodai kuwa ushamiri wa maambukizi bado ni mkubwa katika mkoa huo. Mheshimiwa Anne Kilango Malecela alisema maambukizi ya UKIMWI katika mkoa wa Shinyanga ni asilimia 7.4 ukilinganisha na maambukizi ya kitaifa ambayo ni asilimia 5.1 ,hivyo kuwataka wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo mashirika ya kijamii kuendeleza jitihada za kuzuia maambukizi mapya VVU.

Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGPAHI Dr. Sekela Mwakyusa akiwa na Meneja Miradi kutoka AGPAHI, Dr. Gastor Njau wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinatolewa na wadau wa maendeleo mkoani Shinyanga.

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

BOFYA MANENO HAYA KUANGALIA PICHA ZAIDI ZA KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI YA MKOA WA SHINYANGA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post