AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA JELA KWA KUSAFIRISHA MAJANI YA MIRUNGI




Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, imemfunga jela maisha mfanyabiashara, Silay Maulid Jumanne (35) baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha kilo 21 za majani ya mirungi.


Hukumu hiyo iliyotolewa jana na Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Aishiel Sumari, ni ya kihistoria katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini kwani haijawahi kutolewa tangu Tanzania ipate Uhuru.


Wengi wa wanaokamatwa na mirungi, hushtakiwa kwa kupatikana na mirungi, shtaka ambalo husikilizwa na mahakama za chini tofauti na kusafirisha ambalo husikilizwa na Mahakama Kuu.


Kutokana na mazoea hayo, washtakiwa wengi wanaopatikana na hatia kwa kosa la kupatikana na mirungi, huishia kupigwa faini hatua inayoelezwa kuchangia kushamiri kwa matumizi ya mirungi.


Hata hivyo, mshtakiwa huyo jana hakuamini masikio yake pale Jaji Sumari alipomweleza kuwa adhabu ya kusafirisha mirungi kama ilivyo dawa nyingine za kulevya ni kifungo cha maisha jela.


Akitoa adhabu hiyo, Jaji Sumari alisema upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tamari Mndeme umejenga kesi hiyo na kuishawishi Mahakama pasi na kuacha shaka.


Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mndeme akisaidiwa na mwenzake Kassim Nassir, ulidai kuwa Septemba 7, 2013, mshtakiwa alikamatwa na vifurushi 21 vya Mirungi.


Kwa mujibu wa mashtaka hayo, mshtakiwa alikamatwa kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi, akiwa kwenye harakati za kusafirisha mirungi hiyo kwenda kuiuza jijini Arusha.


Jaji Sumari alisema ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa mashitaka, umethibitisha kuwa mshtakiwa alikamatwa na begi la rangi ya kijani likiwa na mirungi hiyo.


Alisema licha ya mshtakiwa aliyekuwa akitetewa na Wakili Martin Kilasara, kujitetea kuwa hakukamatwa stendi kuu bali eneo la Majengo mjini Moshi, ushahidi umethibitisha alikamatwa stendi kuu.


“Baada ya kusikiliza ushahidi, mashahidi wamethibitisha ulikamatwa Stendi Kuu Moshi, ushahidi huo uliungwa mkono na kondakta wa basi na dereva teksi aliyekuchukua,” alisema.


Jaji Sumari alisema polisi hawakuwa na sababu yoyote ya msingi ya kumbambikia shtaka mshtakiwa huyo, kama alivyojaribu kujitetea na kusisitiza kuwa ushahidi ulikuwa madhubuti dhidi yake.


“Kulikuwa na tofauti ndogondogo kama begi lilibebwa na nani kutoka stendi, au kutoka kwenye basi kwenda kwenye teksi lakini zilikuwa ni tofauti ndogo hazikuharibu mizizi mikuu ya ushahidi,” alisema.


Kwa mujibu wa Jaji Sumari, ukiacha ushahidi huo, ungamo la mshtakiwa linaongeza nguvu na kushabihiana na ushahidi uliotolewa na mashahidi.


Jaji Sumari alisema mirungi ni dawa za kulevya zenye madhara, ushahidi wa Mkemia Mkuu wa Serikali, ulibainisha matumizi yake humfanya mtumiaji kuwa mtegemezi wa dawa hizo.


“Matumizi ya dawa za kulevya yanaathiri jamii ulim wengu mzima hasa vijana, hivyo sheria hii ilitungwa ikizingatia uhai wa binadamu ndiyo maana imeweka adhabu kali,” alisema.


Jaji Sumari alimweleza mshtakiwa huyo ambaye muda wote alikuwa akijifuta jasho na kunywa maji, kuwa mtu yeyote anayepatikana akisafirisha mirungi na dawa nyingine ni kufungwa jela maisha.


Hukumu hiyo ilionekana kuwa gumzo katika viunga vya mahakama hiyo jana, huku wanasheria wakisema inapeleka ujumbe kwa jamii kutodharau kosa linalohusiana na mirungi.


Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Tawi la Moshi, David Shilatu alisema hukumu hiyo ni ya kwanza kutolewa na ya aina yake Tanzania.


“Kwa sheria zetu hizi na marekebisho yake, mirungi nayo inaangukia daraja la dawa za kulevya, kwa hiyo upande wa mashtaka ukithibitisha ulikuwa unasafirisha adhabu ni kubwa,” alisema Wakili Shilatu.


Shilatu alisema ingawa mshtakiwa anayo haki ya kukata rufaa, lakini hukumu hiyo itoshe kupeleka ujumbe kwa jamii kwamba matumizi ya mirungi na usafirishaji wake ni kosa la jinai nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post