Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ANGALIA PICHA- RAIS MAGUFULI ATOA ZAWADI YA PASAKA KWA WAZEE WANAOLELEWA KATIKA KAMBI YA KOLANDOTO SHINYANGA



Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ametoa zawadi ya pasaka kwa wazee wasiojiweza wanaolelewa Kambi ya Kolandoto iliyopo katika manispaa ya Shinyanga.


Zawadi zilizotolewa kwa ajili ya wazee hao 23 baadhi yao wakiwa ni wagonjwa wa ukoma na watoto 13 ni mbuzi wawili,kilo 100 za mchele na mafuta ya kupikia lita 20 zote zikiwa na thamani ya shilingi 380,000/=.


Akikabidhi zawadi hizo jana kwa niaba ya rais Magufuli,katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Abdul Dachi,aliyekuwa ameambatana na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro na mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna ,alisema rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ameona ni vyema kusherehekea sikukuu ya pasaka kwa kuwapatia zawadi wazee hao ambao baadhi yao ni wagonjwa wa ukoma.


“Kutokana na mheshimiwa rais kuwa na majukumu mengi,amenituma kuwakabidhi zawadi hii ya pasaka,na amesema yuko pamoja na nyinyi ”,aliongeza Dachi.


“Rais Magufuli na familia yake wanaungana na wazee wa Kolandoto kusherehekea sikukuu ya Pasaka,ameomba mpokee zawadi ya mbuzi wawili,kilo 100 za mchele na mafuta ya kupikia lita 20”,alieleza Dachi.


Akipokea zawadi hiyo kwa niaba ya wenzake,mwenyekiti wa kambi hiyo mzee Samora Maganga alimshukuru rais Magufuli kwa kuwakumbuka na kumuomba kuendelea kusaidia wazee katika jamii kwani wanakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo huduma za matibabu katika vituo vya afya.


“Tunamshukuru sana rais wetu,ameonesha kujali wazee,tunamtakia kila heri katika uongozi wake kwani anaonesha kiasi gani yuko pamoja na watu wananchi wake”,alisema mzee Maganga.


Naye mlezi msaidizi katika kituo hicho cha wazee Evodia Ndaka alisema kituo hicho kinakabiliwa na upungufu wa vyumba vya kulala wazee hao kutokana na baadhi ya majengo kuharibika na kusababisha vyumba vilivyopo kutumiwa na wazee zaidi ya mmoja.


Aliiomba serikali kuzifanyia ukarabati mkubwa nyumba za makazi hayo ya wazee kutokana na majengo yake kuchakaa hali inayowafanya waishi kwa wasiwasi mkubwa na kwamba wamekuwa wakilazimika kuzihama wakati wa mvua inaponyesha kutokana na kuvuja huku nyingi kati ya hizo tayari sehemu za kuta zake zimebomoka.



Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Abdul Dachi akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi ya pasaka kwa wazee wanaolelewa katika kambi ya Kolandoto,pichani ni mfuko wa mchele na mafuta ya kupikia



Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Abdul Dachi(aliyevaa suti katikati) akijiandaaa kukabidhi mbuzi wawili kwa mwenyekiti wa kambi ya wazee ya Kolandoto mzee Samora Maganga(aliyeshikilia fimbo kushoto),aliyesimama nyuma mwenye suti ni mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna na mleza msaidizi wa kituo hicho Evodia Ndaka



Zoezi la kukabidhi mbuzi wawili likiendelea,aliyevaa nguo nyekundu ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro,aliyeshikilia mbuzi ni mmoja wa wapishi katika kambi hiyo ya wazee



Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Abdul Dachi akikabidhi mbuzi kwa ajili ya pasaka kwa wazee wanaoishi katika kambi ya wazee ya Kolandoto



Zoezi la kukabidhi mbuzi linaendelea



Wazee wakiwa wameshikilia kamba

Picha/Habari na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com