Jeshi la Polisi mkoani Simiyu limemfukuza kazi askari wake kwa kudaiwa kumtorosha mtuhumiwa wa mauaji katika kituo cha Luguru wilayani Itilima, mkoani Simiyu.
Pia, linawashikila askari saba wanaodaiwa kuwatorosha watuhumiwa wengine watatu wa mauaji na ujangili wilayani Meatu kwa uchunguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Onesmo Lyanga alisema askari huyo amefukuzwa kazi kwa kulifedhehesha jeshi na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
“Februali 2, mwaka huu katika Kituo cha Polisi Lugulu, askari alimtorosha mtuhumiwa wa kesi ya mauaji Itl/Ir/95/2016, mkazi wa Kijiji cha Gambasingu wilayani Itilima,” alida Kamanda Lyanga.
Hata hivyo, alisema polisi wanaendelea kuchunguza tukio la kutoroka kwa watuhumiwa wa ujangili wilayani Meatu, na linaendelea kuwashikilia askari wengine saba.
Alisema tukio hilo lilitokea Januari 19, 2016, usiku katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Meatu mkoani hapa na kusababisha watuhumiwa hao kutoboa ukuta na kutoka.
Kamanda huyo aliwataja watuhumiwa waliotoroka kuwa ni mkazi wa kijiji cha Mwasungula aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji na wengine wawili ni wakazi wa kijiji cha Sapa wanaotuhumiwa kukutwa na pembe za tembo.
“Watuhumiwa waliotoroka katika mahabusu siyo ambao walihusika kutungua helkopita na kusababisha mauaji ya rubani Rogers Gower, raia wa Uingereza kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyo ripoti, watuhumiwa hao wapo,”alisema Lyanga.