Polisi mmoja anadaiwa kumpiga risasi dereva daladala, Pistus Ngowi baada ya kutofautiana kauli.
Tukio hilo lililotokea juzi saa tatu usiku, Kariakoo jijini Dar es Sallam lilisababisha madereva wenzake wanaofanya wote safari za Tandika pamoja na wa Temeke kugoma kwa zaidi ya saa tano wakidai kwamba licha ya kushambuliwa, amebambikiwa kesi katika Kituo cha Polisi cha Msimbazi.
Ilidaiwa kuwa wakiwa katika Mtaa wa Lindi kilipo kituo cha daladala hizo, polisi huyo aliyetajwa kwa jina moja la Dotto akiwa kwenye doria, walitofautiana na dereva huyo kisha kumtolea bastola na kumpiga nayo mkononi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa awali, alipewa taarifa za askari wake kushambuliwa akiwa doria na alimpiga risasi dereva huyo kujitetea.
“Huyu askari yupo mahabusu anahojiwa na polisi ili kubaini chanzo cha tukio hili,”alisema Kamanda Sirro.
Dereva wa daladala aliyeshuhudia tukio hilo, Mateso Elias alidai kuwa walikuwa madereva 15, waliokuwa wakisubiri abiria ghafla walisikia kelele za Dotto akimfokea dereva huyo akidai kuwa alitaka kumgonga alipokuwa akiwasili kituoni hapo.
Alisema ili kuepusha shari, Ngowi alishuka kwenye basi na kumuomba msamaha akiwa amepiga magoti lakini polisi huyo alikataa kumsamehe.
Alisema kitendo hicho kiliwavuta madereva waliokuwapo hapo ambao walisogea eneo hilo kujua kilichokuwa kinaendelea: “Ghafla alitoa bastola na kutuamuru wote tuondoke. Tulipopiga hatua kama hatua tano, alifyatua risasi na kumpiga Ngowi mkononi na nyingine alipiga hewani.”
Alisema baada ya tukio hilo aliwapigia simu askari wenzake ambao walifika na kumpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Social Plugin