Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari katika hospitali ya Hindu Mandal Jijini Dar es Salaam kuelezea maendeleo ya afya yake.
Baada ya katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif kurejea kutoka India alipokuwa anafanyiwa upasuaji wa Mgongo na kwa mujibu wa Daktari wake upasuaji ulifanikiwa na aliporejea alikuwa na afya njema na akapumzika Zanzibar.
Leo March 8 2016 Maalim Seif Sharif amethibitisha jana hali yake ilibadilika ghafla akiwa uwanja wa ndege Zanzibar, alipata kizunguzungu kikali ikabidi asaidiwe kupelekwa kupanda ndege kutoka Zanzibar mpaka Dar es salaam na kisha kulazwa hospitali na leo ameyazungumza haya…
"Nilipofikishwa hapa walikuwa washajitayarisha wamenipokea vizuri sana wakaanza kufanya uchunguzi wao na baada ya muda kama saa mbili tatu hali ikarudi ikatengamaa, nikalala salama usingizi mzuri na nimeamka salama asubuhi nimefanya mazoezi kwa miguu yangu mwenyewe na ninatembeatembea kwa miguu yangu mwenyewe, hali sasa hivi ni nzuri kama kama kawaida",amesema Maalim Seif Sharif
Amesema anaendelea vyema baada ya jana kuugua ghafla na kulazwa katika hospitali hiyo.
Amewashukuru wananchi ndani na nje ya nchi kwa kuonesha mapenzi na ushirikiano makubwa.
Daktari wa Maalim Seif Sharif, Omary Mohamed Suleiman amethibitisha pia kuwa afya ya kiongozi huyo kuwa ni njema na muda wowote madaktari watamruhusu..
"Hakuna kubwa lililoonekana kila kitu kipo sawa, isipokuwa inaonekana ni hali ya uchovu alihitaji mapumziko zaidi na baada ya kufika hapa Hospitali madaktari baada ya uchunguzi wao wakaona bora abakie hospitalini wazidi kumuangalia mpaka kesho yaani leo mpaka sasa hivi hali imeenda vizuri tunategemea wakati wowote ataruhusiwwa kwa mujibu wa madaktari",amesema Omary Mohamed Suleiman