Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BAADA YA WAFUASI 42 WA CUF KUKAMATWA ,MSHAURI WA MAALIM SEIF NAYE AKAMATWA NA POLISI ZANZIBAR



Jeshi la Polisi linamshikilia mwanasiasa Mansoor Yussuf Himid kwa mahojiano kuhusiana na kulipuliwa kwa maskani ya CCM, Kisonge Michenzani mjini Unguja.


Mansoor, ambaye ni mshauri wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad alipigiwa simu jana jioni na polisi kwa ajili ya mahojiano katika kituo cha Madema.


Kukamatwa kwa Mansoor kumekuja siku chache baada ya Jeshi hilo kuwakamata wafuasi wengine 42 akiwamo Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Hamad Masoud akituhumiwa kutoa taarifa kwamba kuna watu wamekimbilia porini na wengine wamekwenda Mombasa.


Wafuasi hao 42 ambao bado wanashikiliwa ni kutokana na kuhusishwa na tukio la kulipuliwa nyumba ya Kamishina wa Polisi, Hamdan Omar Makame.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam jana alithibitisha kukamatwa kwa Mansoor na kwamba ni kutokana na hali ya matukio ya milipuko na mambo mengine, hivyo wanahitaji kupata maelezo ya kina kabla ya kumwachia.


Alisema lengo la kumshikilia Mansoor si kumkomoa bali ni kupata ufafanuzi na maelezo kwani hivi sasa kutokana na hali na matamshi ambayo huwa yanatolewa katika mitandao ya kijamii, Jeshi la Polisi linayafuatilia kwa kina kuyachunguza.


“Kwa hivyo tunataka maelezo na tukishapata maelezo yake tutaamua kama ni kumwachia au la, lakini kwa sasa tunamhitaji kwa kuisaidia polisi kwenye upelelezi,” alisema Mkadam.


Tukio hilo limekuja saa chache baada ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya kulalamikia dalili za wazi za uvunjifu wa haki za binadamu Zanzibar zinazofanywa na vyombo vya dola dhidi ya wafuasi wao kwa kivuli cha utunzaji wa amani.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Sakaya aliisihi Serikali ya Rais John Magufuli kuingilia kati kwani wananchi wanaweza kuchoshwa na vitendo hivyo na kuleta uvunjifu zaidi wa amani.

Sakaya alisema kuwa wanaamini mambo yote hayo yanatokea kutokana na msimamo wao wa kutokubali kushiriki uchaguzi wa marudio unaofanyika Jumapili hii.


Uchaguzi huo wa marudio unafanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutokana na kile alichodai kukithiri kwa ukiukwaji wa taratibu na sheria za uchaguzi.


Sakaya alisema kuwa kuna vitendo vingi wanafanyiwa wafuasi wa CUF visiwani humo vikiwamo vya kupigwa na vikundi vya uhalifu vinavyoitwa ‘mazombi’, kuchomewa nyumba na kutiwa ndani kwa viongozi wa chama hicho kwa visingizio vya kushiriki uhalifu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com