Kitu kinachosadikika kuwa bomu kimeripuka usiku wa kuamkia jana eneo la Michenzani mjini Unguja, eneo linalojulikana kama maskani maarufu ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mlipuko huo umezua taharuki na hofu kwa wananchi wa eneo hilo hususan wanachama wa CCM ambao hukutana kwa wingi eneo hilo na kujadili masuala mbalimbali ya chama chao kuelekea uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.
Naibu Katibu Mku wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alilaani tukio hilo na kulielezea kuwa liliandaliwa makusudi kwa lengo la kuwavunja moyo wanachama wa chama hicho.
“Hili sio tukio la kwanza wala la pili katika eneo hili ambalo wanachama wetu walio msitari wa mbele wako wengi sana kwa kushirikiana na wanachama wengine.
"Hili ni tukio ambalo unaweza kusema limeandaliwa kwa makusudi na watu wenye dhamira ya kuwavunja moyo wanachama wetu na wapenzi wa CCM,” Vuai aliwaambia waandishi wa habari.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibu, Mkadam Khamis Mkadam alieleza kuwa Jeshi hilo liliwasili katika eneo hilo usiku huo na kuimarisha ulinzi hadi asubuhi.
Kamanda Mkadam alisema kuwa walichukua vipande vya mlipuko huo na kuvipeleka sehemu husika kwa ajili ya kuchunguza kubaini aina ya mlipuko huo na vifaa vilivyotumika