James Lembeli |
Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga leo imetupilia mbali maombi ya James Lembeli wa CHADEMA ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini wa Octoba, 25’2015, kwa madai kwamba taratibu zilikiukwa.
Akisoma hukumu iliyochukua saa tatu Jaji wa Mahakama hiyo Moses Mzuna amesema, ushahidi uliotolewa na upande wa Lembeli haukuwa na nguvu za kutosha kuishawishi mahakama hiyo kutengua matokeo ya uchaguzi kwani sehemu kubwa ni wa maneno.
Jaji Mzuna amesema, kitendo cha Lembeli kulalamikia vitendo vya rushwa vidavyodaiwa kufanywa na mgombe wa kiti hicho kupitia Chama Cha Mapinduzi-CCM Jumanne Kishimba kushindwa kuvitolea taarifa kwenye vyombo vya dola kimedhoofisha ushahidi na kuuwekea mashaka.
Kwa upande wa mashahidi waliounga mkono kuwepo kwa vitendo vya rushwa Jaji Mzuna amesema wameshindwa kujenga hoja kwa mlolongo unaofanana kiasi kwamba wameonekana kana kwamba walikuwa na ushahidi wa kutengenewa.
Amefafanua kuwa madai ya unyanyasaji wa wafuasi wake waliokamatwa na polisi katika hoteli ya Golden Rock na wengine katika kata ya Ngogwa yamekosa nguvu kufuatia kukosekana kwa kielelezo cha maandishi kinachoonesha kwamba walikuwa mawakala wake.
Mzuna amesisitiza, sababu ya Lembeli kushindwa kupeleka malalamiko kwenye kamati ya maadili ya uchaguzi iliwekwa kisheria kwamba hakuwa na muda wa kutosha haikubaliki kwa kuwa mpiga kura yeyote anayemuunga mkono angeweza kulalamika.
Kufuatia uamuzi huo wa mahakama kutupilia mbali maombi ya kutengua matokeo hayo Lembeli amesema anaiheshimu mahakama, na kwamba atashauriana na wakili wake kuona kama haki haikutendeka ili kukata rufaa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini aliyekuwa mlalamikiwa namba moja katika shauri hilo Kishimba alipohojiwa amesema Jaji ametenda haki kama walivyotenda haki wananchi wa kahama kwa kumpa kura za ushindi katika uchaguzi wa oktoba 25,2015.
Shauri hilo lilikuwa limevuta hisia za wananchi wa Kahama na kuhudhuria kwa wingi leo kwenye hukumu yake huku makundi ya kisiasa yaani wana-CCM na wana-CHADEMA yakijionesha wazi kwa kushangilia bila dalili zozote za uvunjifu wa Amani.
Social Plugin