Mkurugenzi Mkazi wa shirika la EGPAF nchini Tanzania, Dr. Jeroen Van't Pad Bosch akijitambulisha kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan baada ya kuwasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya Utepe Mweupe kitaifa yaliyofanyika jana yenye kauli mbiu "Vifo vya mama vitokanavyo na uzazi havivumiliki, Wajibika".
Mkurugenzi Mkazi wa EGPAF nchini Tanzania, Dr. Jeroen Van't Pad Bosch akimkaribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika banda la EGPAF.
Mratibu wa mawasiliano na utetezi wa EGPAF, Mercy Nyanda akitoa maelezo ya kazi za EGPAF nchini Tanzania kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan
Afisa mradi wa ushirikishi jamii wa EGPAF Tanzania, Deborah Frank akikabidhi zawadi kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan
Waandamanaji wakiingia katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam kuadhimisha siku ya Utepe mweupe Kitaifa.
*******
Shirika la Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) limeungana na wadau wengine wa kitaifa wa katika maadhimisho ya siku ya Utepe mweupe yenye kauli mbiu: Vifo vya mama vitokanavyo na uzazi havivumiliki, Wajibika.
Maadhimisho hayo yamefanyika jana kitaifa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan.
Mamia ya watu walitembelea banda la EGPAF katika viwanja wa Karimjee na kupata elimu ya afya ya uzazi na jinsi ya kuepuka vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na UKIMWI na VVU.
Akiongea na mgeni rasmi katika banda hilo, mratibu wa mawasiliano na utetezi wa Shirika la EGPAF nchini Tanzania, Mercy Nyanda alisema shirika hilo linapata ufadhili kutoka Serikali ya Watu wa Marekani na linalenga katika kutokomeza Maambukizi ya VVU na UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Nyanda aliongeza kuwa katika kuhakikisha afya ya mama na mtoto inazingatiwa, EGPAF hushirikiana na halmashauri za wilaya katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mtwara, Lindi, Tabora, Shinyanga, Geita, na Simiyu ili kuhakikisha akina mama wajawazito na watoto wanapata huduma hizo.
Alisema EGPAF pia hutekeleza huduma za kufuatilia wagonjwa majumbani kwa kushikikiana na Shirika la Pathfinder International na Shirika la Msalaba mwekundu Tanzania katika mikoa ya Pwani, Mwanza, Tabora na Zanzibar.
Social Plugin