Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HATMA YA ZANZIBAR GIZANI,MASWALI YAIBUKA KILA KONA



Ni swali wanalojiuliza watu wengi, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kumtangaza Dk. Ali Mohamed Shein, kuwa mshindi wa nafasi ya urais kwenye uchaguzi wa marudio uliofanyika Jumapili iliyopita kwa kupata kura 299,982, sawa na asilimia 91.4. 

Ushindi huo umeweka historia ya pekee kwa Zanzibar tangu kurejea kwa uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1995. 

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi huo wa marudio yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, anayemfuata Dk. Shein ni Hamad Rashid Mohamed wa chama cha ADC, aliyepata kura 9,734 sawa na asilimia tatu, huku Maalim Seif Sharf Hamad wa CUF aliyetangaza kususia uchaguzi huo, akipata kura 6,076 sawa na asilimia 1.9. 

Historia inasemaje? 

Tangu mwaka 1995, CUF imekuwa mpinzani mkubwa wa CCM na karibu kila uchaguzi, imekuwa ikitangazwa na ZEC kupata zaidi ya asilimia 40 ya kura zilizopigwa. 

Mwaka 1995, mgombea wa CCM, Dk. Salmin Amour Juma, alitangazwa kushinda kwa kupata kura 165,271 sawa na asilimia 50.2 huku Maalim Seif wa CUF akiwa na kura 163,706 sawa na asilimia 49.8 ya kura 328,977 zilizopigwa. 

Kadhalika, mwaka 2005, Amani Abeid Karume wa CCM alishinda kwa kura 239,832 sawa na asilimia 53.2, huku Maalim Seif akifuatia kwa kura 207,733 sawa na asilimia 46.1. Kura halali zilikuwa 450,968. 

Mwaka 2010, Dk. Shein wa CCM alipata kura 179,809 sawa na asilimia 50.1, Maalim Seif kura 176,338 sawa na asilimia 49.1. Kura halali zilikuwa 358,815. 

Kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010, hali ya kisiasa ya Zanzibar ilikuwa tete, hasa kutokana na viongozi wa CUF na wanachama wake kuamini kwamba kwa miaka yote wamekuwa wakishinda, lakini huibiwa kura. 

Hali hiyo ilijitokeza dhairi Januari, 2001, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, kwa kuibuka vurugu na watu kadhaa kupoteza maisha huku wengine wakikimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya walikokaa kama wakimbizi. 

Baada ya uhasama wa muda mrefu, mwaka 2010 ilipoundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), hali ya kisiasa ya visiwa hivyo ilitulia. 

Miaka mitano baadaye sasa, CUF imesusia uchaguzi wa marudio ikitaka mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 2015 atangazwe, jambo linaloibua maswali mengi juu ya mustakabali wa visiwa hivyo. 

Hali ya Muungano 
Kwa muda mrefu Wazanzibar wamekuwa wakilalamikia mfumo wa Muungano, hali iliyofanya wakati wa mchakato wa Katiba Mpya wengi kupendekeza kuwa na Muungano wa Mkataba. 

Hata hivyo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilitokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba, ilipendekeza kuwa na Muungano wa Serikali Tatu ambazo zilionekana kuungwa mkono na Wazanzibari, waliokuwa wanataka mfumo wa mkataba. Lakini suala hilo liliota mbawa, baada ya Katiba Inayopendekezwa kulitupilia mbali. Swali, ni je, baada ya uchaguzi huu, hali itakuwaje? 

Zanzibar yenye mamlaka kamili 
Hoja ya Zanzibar yenye mamlaka kamili, imekuwa pia ikishinikizwa kwa muda mrefu na chama hicho cha upinzani, ambacho kwa mujibu wa matokeo hayo ya ZEC kwenye uchaguzi uliopita, yanaonyesha kimekuwa kikiungwa mkono na zaidi ya asilimia 40 ya watu wanaopiga kura. 

Chama hicho kutokuwa na mwakilishi hata mmoja kwenye baraza la wawakilishi wala kiongozi serikalini, kunaweza pia kufanya hoja hiyo sasa ikashika kasi, kutokana na kuamini kwamba kurudiwa kwa uchaguzi huo kumetokana na shinikizo la Tanzania Bara. 

Waziri wa Fedha wa SMZ, Omary Yusuph Mzee, akizungumza na Nipashe mapama wiki hii, ofisini kwake eneo la Vuga, Zanzibar, alisema lengo la serikali ni kuhakikisha inaondokana na utegemezi wa wafadhili. 

Mzee alisema Zanzibar inategemea asilimia 20 ya misaada kwa ajili ya kukamilisha bajeti yake kila mwaka pamoja na mikopo kutoka taasisi za fedha, zikiwamo benki za nje. 

Pia bajeti ya Serikali ya Zanzibar inategemea asilimia 20 ya mikopo kutoka nje, jambo ambalo litaweza kuathiri maendeleo ya visiwa hivyo, endapo nchi wahisani zitaweka mgomo kwa sababu ya uchaguzi huo. 

Kauli hiyo ya Mzee inaibua swali la kwamba baada ya wahisani kuonyesha kutoridhishwa na uchaguzi ulivyokuwa, nini hatma ya visiwa hivyo endapo wakisusia kuchangia bajeti yake? 

Utalii 
Alisema bajeti ya Zanzibar inategemea asilimia 26 hadi 28 ya mapato yanayotokana na sekta ya utalii wa ndani na nje na kwamba bado kunahitajika mikakati ili kupanua wigo wa kupata fedha. 

Kwa mujibu wa Mzee, Zanzibar inapokea watalii kati ya 300,000 na 400,000 kwa mwaka na kwamba wanatarajia wataongezeka baada ya kufungua ofisi za kuhamasisha utalii wa nje. 

Licha ya takwimu hizo kuonekana ziko juu, hali ya sasa ya takriban asilimia 50 ya Wazanzbiar ambao wanaunga mkono CUF kususia uchaguzi wa marudio, je hakutaathiri sekta ya utalii haswa ikitegemeana na historia ya miaka ya nyuma kabla ya muafaka kufikiwa? 

Wasomi wachambua 
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jijini Dar es Salaam, Prof. Haji Semboja wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), alisema utawala wa Zanzibar haukuwa halali kushikiliwa na CCM, kutokana na mwitikio mkubwa wa ushindi ulioonyeshwa na CUF. 

“Rekodi ya uchaguzi uliopita inaonyesha vyama vya upinzani vilistahili ushindi kwa Tanzania Bara na Visiwani tofauti na awali, kwa sababu kama vimeweza kutoka asilimia 10 za ushindi na kuingia nafasi ya kinyang’anyiro, kisiasa vilistahili kushika madaraka kama dhamira ya serikali ni kuwa na vyama vingi,” alisema Prof. Semboja. 

Alisema ingawa mfumo wa kiuchumi hautayumba kwa serikali hizo mbili kutokana na madaraka hayo kushikiliwa na CCM, bado mfumo wa kidemokrasia utaathiri vyama vinavyothubutu kushiriki uchaguzi, kwa sababu wananchi wanataka mabadiliko. 

Katika hilo, alimshauri Dk. Shein, kufanya majadiliano na vyama vya upinzani ili kuwapo na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. 

“Kwa sasa washirikiane wakae meza moja na kupanga maendeleo ya serikali yao, lakini CCM wawe wapole na CUF wawe wastaarabu kwa maridhiano ya pamoja kwa sababu nchi yetu ni moja, tujenge umoja wetu,” alisema Semboja. 

Naye Prof. Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), alisema kama jitihada za haraka hazitafanywa na viongozi wa ngazi za juu, akiwamo Maalim Seif, kuunganisha umoja wa wananchi, hali ya mauaji inaweza kujitokeza. 

Alisema uchaguzi si tendo la kuhesabu kura na kushinda, bali ni tendo la kisiasa ambalo ndani yake linaunganisha muungano wa wananchi, hivyo uchaguzi ukiwagawa wananchi katika matabaka, inamaanisha uchaguzi huo ni batili kwa sababu haujaunganisha lengo moja. 

Kwa mantiki hiyo, uchaguzi unaogawa wananchi na kuweka sura ya mpasuko si sahihi wala haujatumia haki kwa sababu hautajenga maendeleo na badala yake utabomoa,” alisema Prof. Baregu. 

Alisema uchaguzi wa marudio, uliofanywa Zanzibar Machi 20, mwaka huu, na kwa mara nyingine Dk. Shein kushinda urais kupitia CCM, umewapa ubumbuazi na kuwapiga ganzi Wanzanzibar wengi, kwa sababu tatizo kubwa ni uhalali wa rais aliyeshinda kwa wananchi. 

“Ukifuatilia uchaguzi wa Oktoba, mwaka jana, mshindi hakutangazwa, na baadaye uchaguzi huu baadhi ya vyama vimejiondoa. 

Kutakuwapo na hali ya kutoelewana kwa sababu uchaguzi huo, kulisababisha mtafaruku kwa Wazanzibari tangu awali, hivyo mgogoro ni jambo lisilozuilika kwa sasa Zanzibar,” alisema. 

Aliongeza kuwa: “Mawasiliano ni jambo la busara kwa nchi yoyote yenye kupenda amani na taifa lake. Ushauri wangu serikali ya Zanzibar itafute njia ya kukaa na vyama vya siasa ili kuingilia kati hali ya mvutano unaoendelea kwa sababu wakipuuza jambo dogo waelewe hali ya uvunjivu wa amani inaweza kujitokeza na mauaji yataendelea,” alisema. 

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Paul Kuwenga, alisema suala la Zanzibar linahitaji kuangaliwa upya kwa sababu liko katika kipindi cha mpito wa vyama vingi. 

Alisema kinachotakiwa ni ushirikishwaji kwa sababu jamii inayoishi humo ni mchanganyiko na kila moja ina uhuru wa kufanya uamuzi wake katika jambo fulani, badala ya kushinikizwa wakubaliane kwa sababu nchi iko katika utawala wa demokrasia. 

KAULI YA DK. SHEIN AKIAPISHWA 
Jana Zanzibar iliweka historia nyingine kwa wananchi wake kushuhudia Rais wa awamu ya saba, Dk. Shein akila kiapo cha kuongoza visiwa hivyo. 

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othuman Makungu, alimwapisha Dk. Shein saa tano asubuhi, ikifuatiwa na tendo la kupigiwa mizinga 21. 

Dk. Shein ambaye aliingia uwanjani hapo akiwa na msafara wa magari 10 na pikipiki 13, kabla ya kula kiapo, alikagua gwaride maalum la majeshi ya ulinzi na usalama. 

Rais huyo wa Zanzibar akizungumza baada ya kuapishwa, aliahidi kuongoza kwa haki na bila kumwonea mtu yeyote. 

Aliwataka Wazanzibari kudumisha amani na umoja ili kuharakisha kujiletea maendeleo yao, huku akisisitiza kwamba uchaguzi umekwisha. 

Alisema atahakikisha amani inadumishwa na kwamba atavishughulikia vikundi vyovyote vitakavyojaribu kufanya vurugu visiwani humo. 
Pia aliahidi kuunda serikali makini ambayo itawasaidia Wazanzibari kujiletea maendeleo ya haraka, huku akisema afanya hivyo kwa kuangalia Ilani ya CCM ya mwaka 2015. 

Dk. Shein alisema Zanzibar ina matatizo mengi na kwamba serikali makini itasaidia kutatua matatizo ya wananchi wake. 
Aliwapongeza wapigakura ambao walimchagua na kusema kipaumbele chake ni kuhakikisha amani inatawala visiwani humo na kwamba serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayejaribu kuvunja amani. 

Aliwaomba viongozi wa dini kuhubiri amani na kwamba serikali yake itahakikisha inawaunganisha Wazanzibar wote bila itikadi za vyama vyao. 

AHADI YA SHEIN KWA MAGUFULI 
Dk. Shein alimwahidi Rais John Magufuli kwamba atashirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusimamia misingi ya uwajibikaji na kuhakiksha watumishi wa umma wanakuwa na nidhamu. 

"Nitaunda serikali makini ambayo inafuata maadili na hili nitahakikisha linafanyika haraka iwezekanvyo,” alisema. 

Kabla ya kula kiapo, Dk. Shein aliombewa dua na viongozi wa dini, akiwamo Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Khamis Haji Khamisi na Askofu wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Augstine Shao na Askofu wa Kanisa la Anglikana, Michael Hafidh. 

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Magufuli, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, Marais wastaafu na wananchi wa kawaida. 

Viongozi wa chama kikuu cha upinzani cha CUF pamoja na wafuasi wao hawakuhudhuria sherehe hizo.

CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com