Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HII NDIYO KAULI NZITO YA MBOWE KUHUSU UCHAGUZI WA MEYA DAR



Mwenyekiti mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
Freeman Mbowe amesema kuwa, umoja huo kamwe hautaomba Umeya wa Jiji la Dar es Salaam bali watadai.


Amesema, Jeshi la Polisi linafanya hujuma kwa kuzuia mikutano pamoja na kukamata wabunge pia madiwani wa Ukawa na kwamba, hiyo ni mikakati ya kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda uchaguzi wa umeya Dar es Salaam.


Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema-Taifa amesema umoja huo haupo tayari kushiriki uchaguzi wa Meya kwa kushtukiza akidai kuwepo kwa mkakati huo.


Amesema hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho na kwamba, mara zote wamekuwa wakitaarifiwa kwa kushitukiza ili wasipate muda wa kujiandaa.


“Sasa tumechoka kuwabembeleza, mara zote huwa tunafanya kwa kuheshimu maamuzi yao hata kama wanavunja katiba,” alisema Mbowe na kuongeza;


“Jana ( juzi) wabunge na madiwani wetu walienda kwa Mkurugenzi wa Jiji kwa lengo la kutaka kujua tarehe ya uchaguzi, lakini hatukupata, kwa kuwa tumeshaomba hawataki sasa tutakachoamua tusilaumiane. Tumechoka kudai haki kwa kubembeleza na sasa hatutaomba tena.”


“Tunakosa imani na viongozi wa kiserikali na Jeshi la Polisi kwa ujumla juu ya utendaji wake na kutokana na yanayoendelea yakiwemo ya viongozi wetu wa chama kukamatwa tunapata wasiwasi inawezekana polisi ni vibaraka wa (CCM),”amesema Mbowe.


Akieleza baadhi ya maazimio ya Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichokaliwa tarehe 1 Machi mwaka huu alisema, kilitafakari utendaji wa Rais John Magufuli na kubaini kuwa, serikali yake inavunja misingi ya utawala bora ikiwemo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushindwa kusimamia majukumu yake.

Alisema chama kinaandaa mkutano mkubwa utakaofanyikia Mwanza ambao utashirikisha viongozi wa nchi nzima pamoja na wabunge kwaajili ya kujadili hali ya chama na jinsi ya kujipanga kwa uchaguzi wa mwaka 2030.Mkutano unatarajiwa kuanza tarehe 13 Machi mwaka huu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com