Wakati wengi wakizidi kuhoji uwezo wa Katibu Mkuu mpya wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, kutokana na kutokuwa na jina kubwa katika uwanja wa siasa, mbali na elimu aliyonayo, kipaji chake na uwezo binafsi, vimezidi kufichuka.
Mwishoni mwa wiki, Chadema ilimteua Dk. Mashinji kuwa Katibu Mkuu mpya kushika nafasi ya Dk. Wilbroad Slaa aliyejiuzulu nafasi hiyo Julai 30, mwaka jana kwa kile akichodai kuwa ni utaratibu kutofuatwa wa kumkaribisha Edward Lowassa, aliyehamia katika chama hicho kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kisha kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia chama hicho akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hata hivyo, wakati wengi wakihoji uwezo wake, imefahamika kuwa Dk. Mashinji kwa kushirikiana na kamati yake, ndiyo waliobuni kaulimbiu (slogan), ya `Lowassa Mabadiliko, Mabadiliko Lowassa,' ambayo ilitumika katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana na kuwa kivutio kikubwa.
Akihutubia mamia ya wananchi wa Jiji la Mwanza katika viwanja vya Furahisha, Katibu Mkuu huyo, alisema: "Katika mkakati wetu kama kamati ya wataalam, tulileta kauli ya Mabadiliko Lowassa, Lowassa Mabadiliko, wameiiga, lakini hawawezi kuwa kama sisi, tunamaanisha mabadiliko tunayoyazungumzia na tutayatekeleza kimkakati na kimfumo zaidi."
Kauli hiyo ambayo hadi sasa inatumika kwenye vikao vya ndani, nje na mikutano ya hadhara vya Chadema, alishirikiana na Kamati ya Wataalam ya Ukawa ambayo imekuwa ikibuni na kushauri mambo mbalimbali ya uendeshaji wa umoja huo.
Katika umoja huo unaohusisha vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, kamati ya wataalam iliongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu na Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania, Dk. Rodrick Kabangila na Makamu akiwa Dk. Mashinji na Katibu alitoka CUF.
Dk. Kabangila, alisema alikutana na Dk. Mashinji Chuo Kikuu cha Makerere, nchini Uganda, akiwa mwaka wa tatu naye wa pili, wakishirikiana kwenye uongozi wa Umoja wa Wanafunzi wa Tanzania wanaosoma chuoni humo.
Baada ya kurudi nchini walikutana tena Muhimbili na kuendelea kushirikiana ikiwamo kuandika majarida mbalimbali ambayo walimpelekea Mbowe kwa ajili ya utekelezaji.
Anasema mwaka 2011, baada ya kujiondoa katika Chama cha Madaktari nchini, baada ya kuona mgongano mkubwa na kutoeleweka katika wanayoyapigania, aliingia kwenye siasa na kwa pamoja waliwekwa kwenye Kamati ya Afya ya Chadema, yeye akiwa mwenyekiti na Mashinji akiwa makamu mwenyekiti.
Alisema baada ya kufanya vizuri kwenye kamati hiyo, walipewa Kamati ya Maandalizi ya Ilani ya Chadema, nako alikuwa mwenyekiti na mwenzake makamu.
Amponda Dr. Kigwangalla
Dk. Kabangila, alimshangaa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Hamis Kingwangala, ambaye amendika kwenye ukurasa wake wa Facebook akimponda Dk. Mashinji, na kwamba wakati wa mgomo wa mwaka 2005 alikuwa ni mwanafunzi aliye katika mafunzo ya vitendo (internship) na kwamba mgomo huo uligawanyika katika maeneo matatu ya wanafunzi wanaofaya mafunzo kwa vitendo, daraja la kati na wakongwe, na kwamba Dk. Mashinji alikuwa katika daraja la juu na alisimamia masuala ya ngazi hiyo.
Alisema katika mgomo wa mwaka 2011, walikuwa na Dk. Kigwangalla, yeye (Kabangila) akiwa ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Madaktari Tanzania na Makamu wa Rais, na walishirikiana wote na Dk. Mashinji kwa kuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa na misimamo thabiti, mtendaji makini na mfuatiliaji wa mambo.
"Namshangaa sana Dk. Kingwangalla, sijui ni siasa inamlevya au baada ya kuwa waziri anasahau kabisa jinsi walivyopambana kuboresha sekta ya afya na maslahi ya madaktari nchini, unapokuwa mtaalam unapaswa kupinga kitaalam na siyo kusema mambo kirahisi rahisi na pasipokuwa na taarifa kamili, kwa sasa inaonekana amesahau kabisa udugu wa kitaaluma tuliofundishwa na tunapaswa kuuhubiri. Ukweli anaujua ila anajilazimisha kutoujua," alisema.
Social Plugin