Kijana aliyejulikana kwa jina la Dotto Paul Shija(21) mkazi wa Uzogore katika manispaa ya Shinyanga ameuawa kwa kupigwa kitu chenye ncha kali kichwani kisha kuvunjwa mguu wake wake wa kulia siku ya mkesha wa pasaka baada ya kutoka disko.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Dismas Kisusi alisema marehemu alifariki dunia Machi 27,2016 saa 4:10 asubuhi katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
Akielezea tukio hilo kamanda Kisusi alisema Dotto Paul Shija alijeruhiwa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na kuvunjwa mguu wake wa kulia katika eneo la Ndembezi Mbalaji katika manispaa ya Shinyanga na watu wasiojulikana.
Alisema awali marehemu alikuwa disko maarufu kwa jina la Mwanamindi iliyokuwa inafanyika katika eneo hilo.
“Ilipofika majira ya saa tisa usiku,marehemu alimuaga rafiki yake aliyekuwa naye Joseph Ajusta(21) mkazi wa Ibadakuli kuwa anakwenda nyumbani kulala,wakati anakwenda nyumbani aliongozana na Emmanuel Hamis(19) mkazi wa Ibadakuli”,alieleza Kamanda Kisusi.
“Palipopambazuka marehemu alikutwa eneo la relini Ndembezi akiwa anavuja damu,akakimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu lakini ilipofika saa 4:10 asubuhi akafariki dunia”,aliongeza kamanda Kisusi.
Hata hivyo alisema tayari jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia Emmanuel Hamis aliyeongozana na marehemu kwa mahojiano zaidi.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Social Plugin