Siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kuwasimamisha kazi wauguzi watano wa Hospitali ya Butimba wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza kufuatia uzembe uliopelekea vifo vya watoto mapacha, madaktari wa hospitali hiyo jana waligoma kwa saa kadhaa.
Madaktari hao waligoma kutoa huduma kwa zaidi ya saa sita na kusababisha usumbufu mkubwa, wakidai kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na kutishwa na watu wanaofika hospitalini hapo kupata huduma.
Akieleza sababu ya mgomo huo, Bi. Rechungula ambaye ni mmoja kati ya watoa huduma ya afya katika hospitali hiyo alisema kuwa wagonjwa wamekuwa wakikiuka taratibu za kupata huduma huku wakiwatishia na kuwasukuma kufanya kazi zao.
“Wagonjwa wanakuja hawataki kufuata utaratibu, wakifika mlangoni wanataka kuandikiwa kadi mara moja bila kufuata utaratibu. Na wakifika kwa daktari vivyo hivyo." Alisema Bi. Rechungula
Alisema kuwa wagonjwa wamekuwa wakiwatishia kuwapiga endapo hawatawahudumia kwa muda wanaoutaka.
Kufuatia sakata hilo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga alifika hospitalini hapo na kuwahakikishia usalama wauguzi hao, huku akitahadharisha watu wanaotaka kuhatarisha usalama.
Alisema kuwa hakutakuwa na sababu ya kuweka ulinzi wa polisi kusimamia huduma hospitalini hapo bali hali ya amani inapaswa kuzingatiwa.
Baada ya kufanya kikao na wauguzi hao pamoja na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, huduma zilirejea hospitalini hapo majira ya saa saba mchana.
Social Plugin