Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAKA AMUUA KWA KISU KIJANA ALIYENG'ANG'ANIA KUCHUKUA DADA YAKE KWA NGUVU BAA SHINYANGA




Siku moja tu baada ya kijana kuuawa kwa kupigwa kitu chenye ncha kali kichwani kisha kuvunjwa mguu akitoka disko siku ya mkesha wa pasaka,kijana mwingine ameuawa kwa kuchomwa kisu akilazimisha kuchukua dada wa mtu aliyejulikana kwa jina la Emmanuel Shombe katika baa ya Matunu mjini Shinyanga.


Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Dismas Kisusi amesema  tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo saa 6:09 usiku katika eneo la Matunu Baa iliyopo mtaa wa Kaunda kata ya Shinyanga mjini.


Kamanda Kisusi amemtaja aliyeuawa kuwa ni Jumanne Ramadhani(22) mwendesha bodaboda mkazi wa Ndala katika manispaa ya Shinyanga ambaye alichomwa kisu kifuani upande wa kushoto na Emmanuel Shombe(20) mkazi wa Majengo na mfanyakazi wa kampuni ya Mobisolar inayojihusisha na uuzaji wa solar.
Amesema chanzo cha tukio hilo ni marehemu kutaka kumchukua kwa nguvu dada yake na Emmanuel Shombe aitwaye Ester Shombe(18) mkazi wa Majengo mjini Shinyanga.

“Marehemu alikuwa analazimisha kumchukua kwa nguvu Ester Shombe,ndipo kaka yake Emmanuel Shombe akachukua kisu na kumchoma nacho kifuani upande wa kushoto kulikomsababishia kuvuja damu nyingi,na alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali”,ameeleza Kamanda Kisusi.

Amesema tayari jeshi la polisi linawashikilia watu wanne kwa ajili ya mahojiano zaidi juu ya tukio hilo ambao ni Emmanuel Shombe,Ester Shombe,Joseph Amos na Tausi Mathias. 
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com