Wasichana wanaovaa nguo fupi za kubana na wavulana wanaovaa milegezo jijini Mbeya , juzi walipata wakati mgumu baada kundi la vijana kuwavua nguo zao na kuzichana hadharani, kutokana na gari la matangazo kupita jijini hapa likiwataka watu kuvaa nguo za heshima zinazoendana na maeneo husika.
Tangu Machi 7 hadi 9, gari la matangazo ya Kampuni ya Studio H ya Huruma lilipita mitaa mbalimbali ya jijini Mbeya, likiwataka wasichana kuacha kuvaa vimini na vijana kuacha kuvaa mlegezo.
Baada ya tangazo hilo, vijana walianza kuwavamia wasichana na wavulana waliovaa milegezo maeneo ya Uyole, Soweto, Kabwe na Mwanjelwa, huku wanawake waliokuwa wakiuza matunda wakiwarushia vitenge wasichana waliochaniwa nguo ili wajisitiri.
Ofisa Habari Jiji la Mbeya, John Kilua alisema uongozi hauhusiki na tangazo hilo.
Hata hivyo, Ofisa wa Kampuni ya Studio H ya Huruma, Siyata Mbua alisema walitoa tangazo hilo baada ya kukamilika kwa makubaliano baina ya jiji na kampuni yake.
Mbua alisema kazi ya kuzuia nguo zisizo za heshima inahusu Serikali, lakini kampuni iliamua kujitolea kwa makubaliano na jiji kwa mwaka mmoja.
“Lengo ni kuwahamasisha wananchi wavae nguzo za heshima. Hatuwahamasishi vijana wawavamie watu, bali tunawataka kila mmoja avae nguo kulingana na maeneo anayofanyia kazi,”alisema. Mabua alisema lengo ni kuelimishana zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema hajapata malalamiko na kuwataka vijana kuheshimu utu wao kwa kuvaa nguo za heshima.
Social Plugin