Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKURUGENZI WA WILAYA YA MASWA AFARIKI KABLA YA WAZIRI MKUU KUMFIKIA, IMEBIDI AKATISHE ZIARA YAKE HUKO SIMIYU

 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekatisha ziara yake ya siku sita mkoani Simiyu, baada ya kifo cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa (DED), Trasias Kagenzi kilichotokea juzi usiku.

Kaimu Katibu Tawala, Donatus Weginah alithibitisha kutokea kifo cha mkurugenzi huyo wakati Waziri Mkuu akiwa na ratiba ya kutembelea wilaya hiyo.

Weginah alisema juzi asubuhi Kagenzi alikuwa akifanya mazoezi ya kukimbia akiwa na mlinzi wake na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Rosemary Kirigini lakini alianza kujisikia vibaya.

“Mkurugenzi alikuwa akifanya mazoezi ‘jogging’ na DC Rosemary Kirigini, lakini baadaye alimwambia Kirigini najisikia pumzi zinabana, akamwambia aendelee… lakini mara mkuu wa wilaya alimuona amejiinamia, aliporudi kumuuliza akamwambia naona nakosa hewa, ndipo alipoamua kukimbia kuchukua gari kumpeleka hospitalini,”alisema.

Weginah alisema mkurugenzi huyo alipelekwa hospitali na majira ya saa tano asubuhi alionekana akiendelea vizuri, hata hivyo baadaye hali ikabadilika mchana na waliamua kumpeleka katika Hospitali ya Bugando kwa uchunguzi zaidi, lakini usiku wa saa saba alifariki dunia.

Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Tawala huyo, alisema mkurugenzi ana kama mwaka mmoja na nusu tangu alipohamia wilayani humo na kwamba familia yake iko Arusha.

Weginah alisema jana mchana mwili wa Kagenzi ulichukuliwa hospitalini Bugando na kuletwa wilayani Maswa ambapo leo asubuhi Waziri Mkuu Majaliwa ataongoza kuaga mwili wa mkurugenzi huyo, lakini baadaye wataangalia familia inaamuaje maana ilikuwa imebaki Arusha, kisha mambo mengine yatafuata.

Via>>Habari Leo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com