Hali ya sintofahamu imeibuka katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru baada ya mtoto mchanga wa siku tano kuibiwa wodini katika mazingira ya kutatanisha.
Tukio hilo limezusha hofu kwa baadhi ya wazazi waliojifungua katika wodi ya wazazi hospitalini hapo wakihofia usalama wa watoto wao na kuomba Serikali kuingilia kati.
Akisimulia tukio hilo, mama mzazi wa mtoto huyo, Sinyari Lucas ambaye ni mkazi wa Simanjiro mkoani Manyara, alisema lilitokea usiku wa kuamkia jana.
Akizungumza huku akiwa ameghubikwa na huzuni, Lucas alisema wakati akiwa kitandani muda wote kabla ya kulala alikuwa na mtoto wake.
Mumewe, Lucas Ngaraa alionyesha kushangazwa na tukio hilo kwa sababu hospitali hiyo ina ulinzi wa kutosha.
Baadhi ya wazazi waliokuwapo kwenye wodi hiyo, walisema muda wote mzazi huyo alikuwa amelala kitandani na mtoto wake, lakini usiku walishangaa kumsikia anapiga kelele.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Jackline Urio alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba, uongozi umelipokea kwa mshtuko mkubwa na unalifanyia kazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema wamepokea taarifa hizo na tayari ameagiza maofisa kwenda kufuatilia tukio hilo kwa kina.
Social Plugin