Mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na DW, Salma Said amedai alitekwa na wanaume wawili baada ya kumkamata na kumuingiza kwenye gari lao kisha kuondoka naye na kumpeleka kusikojulikana.
Salma aliyetekwa Ijumaa iliyopita na watu hao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea Zanzibar kwa ajili ya kuchunguzwa afya yake kwenye moja ya hospitali za jijini Dar, alisimulia mkasa huo jana mbele ya waandishi wa habari huku akimwaga machozi.
Alisema alipoteremka uwanjani hapo, alimpigia simu dereva wake amfuate na wakati akimsubiri, ndipo wakatokea watu hao.
Salma alisema watu hao walimfunga mtandio wake mweusi usoni ili asibaini mahali walikokuwa wakimpeleka na kumfungia chumbani .Alisema ndani ya chumba hicho kulikuwa na vitambaa.
“Waliponiingiza ndani ya chumba kile siku ya kwanza, wakanifungua tambala usoni kwa hivyo nikawaona nyuso zao, mmoja alikuwa na kovu shavuni, mrefu na mwingine mweupe kidogo, waliniweka kule ndani bila kupata chakula chochote,” alisema.
Salma alisema alitakiwa kurudi Zanzibar kwa ajili ya kuripoti marudio ya Uchaguzi Mkuu wa marudio uliofanyika juzi, lakini alishindwa baada ya watu hao kumteka na kumfungia kwenye chumba hicho.
Alidai kuwa watu hao walimwambia watamuachia baada ya uchaguzi huo kufanyika na mgombea wa CCM kutangazwa kuwa mshindi.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za Baraza la Habari Tanzania(MCT), Salma aliongozana na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Bara (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, ambao kwa pamoja walieleza kupinga ukatili huo huku wakiliomba Jeshi la Polisi kuwasaka wahalifu waliohusika.
“Walinisababishia maumivu makali, walinipiga mabuti na makofi huku wakiniambia maneno ya vitisho kama ilivyokuwa kwa Dk Ulimboka na Kibanda,” alidai Salma.
Kabla ya watekaji hao kumrudisha katika eneo walilokuwa wamemteka, Salma alidai kuwa watu hao walimpiga kila walipoingia na kutoka nje ya chumba alichowekwa na kumsababishia apumue kwa tabu.
Akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kupata ufafanuzi wa taarifa za uvumi wa kujiteka mwenyewe, Salma alijibu swali hilo huku akidondosha machozi: “Hakuna sababu ya kusema uongo, mimi ni Mwislamu na dini yangu inakemea kufanya hivyo.”
Pia, alisema amefanya kazi kwa miaka zaidi ya 20 na matukio ya vitisho yalianza alianza kuyapata muda mrefu kwa kupigiwa simu, kutumiwa meseji na kufuatwa nyumbani kwake.
Salma ambaye alizungumza huku akionyesha ushahidi wa meseji za makundi ya mitandao yanayojadili kufurahishwa na kutekwa kwake, alisema kujiteka ni kauli zisizokuwa na uhusiano wowote na ukweli, kwani alijitambulisha kuwa mwandishi mtetezi wa haki za binadamu na siasa ambazo zinazokinzana na maslahi ya wachache.
Wakati huohuo; Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alisema ni mapema kuzungumzia tukio la kutekwa kwa Salma kwa madai kuwa bado wanaendelea kufanya uchunguzi.