Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDEGE YAKAMATWA IKISAFIRISHA NYANI TANZANIA,WAZIRI MAGEMBE ACHARUKA,HAYA NDIYO MAAMUZI YAKE


Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe leo amemsimamisha kazi mkurugenzi mtendaji wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Juma Mgoo pamoja na vigogo wengine wawili kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya uvunaji wa kasi wa misitu pamoja na usafirishaji wa magogo.



Wakurugenzi wengine waliosimamishwa kazi leo ni pamoja na Zawadi Mbwambo (Mratibu wa Maliasili) na Nurdin Chumuya (Mipango na Matumizi ya Rasilimali). 



Kwa upande mwingine, Prof Maghembe amemfuta kazi mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Wanyamapori Dk Charles Mulokozi kwa kuwezesha upatikanaji wa kibali cha kuwasafirisha nyani 61 kwenda Albania huku uchunguzi ukionyesha badala ya idadi hiyo, wanyama kama hao 300 walikamatwa pasipo kibali cha uwindaji. 
"Jana usiku tumekamata ndege ambayo ilikuwa inasafirisha nyani, inaonekana ni biashara inayofanywa kwa hiyo amesimamishwa kazi, uchunguzi ufanywe ili tuone hili jambo la kusafirisha wanyama nje ya nchi limefanywa kiasi gani na ni nani anafanya",alisema

Kwa mujibu wa waziri huyo, ripoti ya ukaguzi uliofanywa na TFS, imebainika ukiukwaji mkubwa hususani katika makusanyo ya mapato na uvunaji magogo usiozingatia sheria za nchi.


Amebainisha kuwa, wakati mwingine watendaji wa misitu walikuwa wakidanganya juu ya mapato halisi yaliyokuwa yanapatikana katika sekta ya misitu.



“Inapofikia wakati unakusanya mapato na ama kupeleka benki pungufu au kutopeleka kabisa kwa zaidi ya mwaka na wakati mwingine taarifa za kibenki zinakinzana ….hii ni aibu kubwa sana,” Waziri Maghembe amesema.


Profesa Maghembe amesema ripoti hiyo imefichua kuwa mkoa wa Rukwa unaongoza kwa uvunaji haramu wa magogo hususani wilayani Kalambo.


“Walichokuwa wanakifanya ni kwamba baada ya uvunaji, magogo yalikuwa yakipelekwa Zambia na kurudishwa Tanzania tena ili kudanganya kuwa magogo hayo yamevunwa nchini Zambia.


“Niliwasiliana na maofisa wa juu wa TFS na nilisubiri wachukue hatua lakini hakuna kilichofanyika,” kwa hasira waziri Maghembe amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com