RAIS MAGUFULI AFIKA KIJIJINI KWAKE,AWATAKA WATANZANIA KUFANYA KAZI KWELI KWELI ILI KUEPUKA MISAADA YA WAFADHILI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefika nyumbani kwake katika kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais, ambapo akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Chato, ametoa wito kwa kila mtanzania kuchapa kazi kwa juhudi ili nchi iondokane na utegemezi wa misaada ya wafadhili ambayo huambatana na masharti.


Dkt. Magufuli amesema jukumu kubwa lililo mbele ya watanzania kwa sasa, ni kushikamana na kujisimamia katika maendeleo ili kila mmoja ahakikishe anaongeza uzalishaji na utendaji kazi mahali pake pa kazi.


"Kwa hiyo ni lazima tujisimamie sisi wenyewe, na tukijisimama sisi wenyewe kwa kila mmoja kuwajibika mahali alipo, kama ni mfanyakazi afanye kazi kwelikweli, kama ni mkulima afanye ukulima wake kwelikweli, kama ni mfanyabiashara afanye biashara kwelikweli, kama ni mfugaji afuge kwelikweli, kama ni mvuvi avue kwelikweli, Tanzania hii tutavuka" Amesema Rais Magufuli.


Aidha, Rais Magufuli amesema serikali yake imeamua kuchukua hatua kudhibiti nidhamu serikalini, kwa kuhakikisha inawachukulia hatua watumishi wa umma wanaolisababishia taifa upotevu mkubwa wa fedha, na ameahidi kuwa hatua hizo maarufu kwa jina la "Kutumbua Majipu" zitaendelea kuchukuliwa hadi tatizo hilo likomeshwe.


Dkt. Magufuli pia amekumbusha viongozi wote wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala na Wakurugenzi, kutekeleza wajibu wao ipasavyo na ameweka bayana kuwa mahali popote ambapo hapatakuwa na ufanisi, kiongozi husika atakuwa amedhihirisha kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa aliopewa.


Rais Magufuli amewapongeza walimu kote nchini kwa kufanya kazi nzuri ya kufundisha, licha ya changamoto ya ongezeko kubwa la wanafunzi waliojiunga darasa la kwanza mwaka huu, lakini ametaka Wazazi na kamati za shule kushirikiana na walimu kuwasimamia wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.


"Niziombe kamati za shule zote Tanzania nzima, kama haziwezi kusimamia nidhamu ya wanafunzi shuleni, zile kamati za shule zijiuzulu. Lakini pia kama wewe ni Mwalimu Mkuu, shule yako kila siku inatoa divisheni ziro nyingi kila mwaka, sioni sababu ya wewe kuendelea kuwa Mwalimu Mkuu" Alisisitiza Dkt. Magufuli.


Kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa, Rais Magufuli amesema uhakiki mdogo uliofanywa hivi karibuni, umebaini wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa shilingi bilioni 1 na milioni 800, na kwamba ni matarajio kuwa uhakiki unaofanywa nchi nzima utaisaidia serikali kubaini wafanyakazi hewa wengi zaidi na kunusuru fedha nyingi zaidi za watanzania.


Ametolea mfano wa mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya watu 17, na kueleza kuwa mfanyakazi huyo atafikishwa mahakamani.


Pia Rais Magufuli amesema serikali yake imejiandaa kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 10 au 9 kuanzia bajeti ijayo, lakini amesema kwa wale wanaolipwa mishahara mikubwa ambayo inafikia hadi shilingi milioni 40, itapunguzwa na kuweka kima cha juu cha mshahara usiozidi shilingi milioni 15.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post