MAMLAKA ya Mawasiliano nchini (TCRA) imeipiga faini ya milioni 10 kampuni ya biashara ya mtandao – RIFARO AFRICA na pia imeizuia kuendelea na huduma kwa madai ya kutokuwa na leseni.
Aidha TCRA imeeleza kushangazwa na taarifa zinazotangazwa katika vyombo vya habari na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa, kampuni hiyo inafanya shughuli zake kutokana na leseni namba 178933 pamoja na cheti cha TCRA namba 15420.
Akizungumza hii leo Makao Makuu ya TCRA Dk. Ally Yahaya Simba Mkurugenzi, Mkuu wa TCRA amesema, baada ya TCRA kuona taarifa hizo za upotoshaji, iliamua kuihoji kampuni ya RIFARO na kuifanyia uchunguzi ambapo walibaini kwamba haina uhalali.
“28 Julai 2014 TCRA ilitoa cheti cha matumizi ya rasilimali masafa kwa ajili ya huduma ya ziada za mawasiliano kupitia SMS namba 15420 ili kutengeneza mfumo wa kuunganisha taarifa za mawakala wao kuuza na kusambaza muda wa maongezi kupitia wavuti.
“Cheti hicho kilimalizika 27 Julai 2015 na kampuni hiyo haikuomba kibali tena cha kuendesha biashara yoyote na hivyo inachokifanya sasa hivi ni kinyume na kanuni ya 17(1) ya Mamlaka ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2011,” ameeleza Dk. Simba.
Ameongeza kuwa, TCRA ilitumia sheria yake sura ya 172 kama ilivyorekebishwa na kifungu cha 179 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta na kuitaka kampuni hiyo ijitetee kwanini ischukuliwe hatua, ambapo ilikiri makosa yake yote.
Makosa ambayo RIFARO AFRICA imekiri katika shauri baina yake na TCRA mnamo 24 Februari 2016 ilipohojiwa ni pamoja na kufanya biashara bila kuwa na kibali, kwani cheti namba 15420 kilikuwa kimeisha muda wake tangu Julai 2015.
Lakini pia RIFARO imekiri kuingia mkataba wa kibiashara na kampuni ya Zanzibar Telecom Limited (ZANTEL) kwaajili ya huduma ya Ezzy Pesa kama mtoa huduma mkubwa “mobile money super dealer” kinyume na sheria.
“Kutokana na makosa hayo tunaitaka RIFARO isitishe mara moja biashara inayoiendesha kwa kutumia rasilimali namba 15420 kwani haina kibali lakini pia tunaipiga faini ya shilingi milioni 10 za kitanzania kwa kuendesha shughuli zake bila kibali”. Amesema Dk. Simba.
Mbali na kampuni hiyo, TCRA pia imeshusha rungu kwa Kampuni ya Azam Marine Company Limited ambayo inamilikiwa na mfanyabiashara Saed Salim Bakhresa kwa kuitaka kuacha mara moja kuendesha shughuli za kiposta za kusafirisha vifurushi na vipeto baada ya kubainika wanafanya hivyo bila kuwa na leseni na kibali cha TCRA, hivyo kuikoseha serikali mapato
Vilevile TCRA imeipiga faini ya shilingi milioni 5 kampuni hiyo kutokana na kufanya shughuli hizo kinyume cha sheria
Social Plugin