Serikali ya Marekani imeamua kutaifisha mali za mfanyabiashara wa dawa zilizopigwa marufuku za kulevya kutoka Tanzania, Ali Khatib Haji Hassan, maarufu kwa jina la “Shikuba” na mtandao wake na kupiga marufuku kampuni za nchi hiyo kujihusisha na biashara zake.
Shikuba, ambaye amekuwa akihusishwa na biashara kubwa ya usafirishaji dawa za kulevya kati ya Afrika Mashariki, Asia, Ulaya na Marekani, alikamatwa mwaka 2014 nchini Tanzania akihusishwa na shehena ya kilo 210 za heroin zilizokamatwa mkoani Lindi mwaka 2012.
Taarifa iliyotolewa juzi na kitengo cha udhibiti wa mali za nje cha Wizara ya Fedha ya Marekani imeeleza kuwa serikali imemtambua Shikuba kama kinara wa usafirishaji wa dawa za kulevya kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi wa Vinara wa Dawa za Kulevya wa Nje (Foreign Narcotics Kingpin Designation Act) ya Marekani.
“Hassan (pichani) ni kinara mkubwa wa kimataifa wa dawa za kulevya ambaye anasafirisha mamilioni ya tani za heroine na cocaine kwenda barani Afrika, Asia, Amerika Kaskazini kwa kutumia mtandao wake uliopo Afrika Mashariki,” inasema taarifa hiyo ya Serikali ya Marekani iliyotolewa Washington juzi.
“Kutokana na uamuzi wa leo (juzi), mali zote za Hassan na mtandao wake ambazo ziko ndani ya mamlaka ya Marekani au kwenye mikono ya raia wa Marekani zinataifishwa.”
Sheria hiyo ya Marekani ilipitishwa mwaka 1999 na kuanza kazi mwaka uliofuatia, ikiwa na lengo la kudhibiti wasafishaji wa dawa za kulevya, biashara na shughuli zao kuingia kwenye mfumo wa kifedha wa nchi hiyo na kudhibiti biashara na miamana baina ya wasafirishaji wa dawa hizo na kampuni za Marekani na raia wake.
Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, sheria hiyo imekuwa ikitumiwa na Marekani kufuatilia wahalifu kadhaa wanaojihusisha na biashara hiyo duniani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Marekani, Hassan amekuwa akijaribu mara kadhaa kurubuni viongozi wa Serikali za Afrika kuepuka kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kutokana na biashara zake haramu.
“Uamuzi wa leo unaweka vikwazo kwa Ali Khatib Haji Hassan na mtandao wake kusafirisha heroine na cocaine duniani na kumzuia kutumia faida haramu kurubuni maofisa wa Serikali za Afrika,” anasema kaimu mkurugenzi wa OFAC, John E. Smith katika taarifa hiyo.
“Wasafirishaji wa dawa za kulevya kama Mtandao wa Usafirishaji Dawa za Kulevya wa Hassan ni tishio kubwa kwa uthabiti wa mfumo wa kimataifa wa fedha na kanda, na Hazina inaendelea kuwa thabiti katika kuuanika na kufuatilia na wale wanaochochea biashara hiyo duniani.”
Tangu mwaka 2006, amekuwa akiongoza wanachama wa mtandao wake kutuma shehena za dawa hizo kwenda sehemu kadhaa duniani kama China, Ulaya na Marekani.
Hassan alikuwa msambazaji wa kwanza kwa wasafirishaji dawa za kulevya wa Tanzania ambao mara kwa mara walikuwa wakipokea maelfu ya kilo za heroine kutoka pwani ya Makran nchini Pakistan na Iran.
Hassan, pia alisimamia mtandao wa wasafirishaji hao barani Amerika Kusini na kuzisafirisha hadi Afrika Mashariki, zikiwa njiani kwenda Ulaya na China.
Akizungumzia hatua hiyo, aliyekuwa Kamishna wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema Hassan alikamatwa Januari mwaka 2014 Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) baada ya mbinu nyingi kugonga mwamba.
“Mtandao wa Shikuba ulikamatwa mapema kabla yake na ilituchukua muda mrefu kumkamata baada ya mbinu zetu nyingi kugonga mwamba,” alisema.
Kuhusu sheria, Kamanda Nzowa alisema iwapo itahakikishwa kuwa Hassan amepata mali zake kwa njia ya kuuza dawa za kulevya, zitataifishwa kama walivyofanya Marekani.