WABUNGE WATATU WAJUMBE WA KAMATI YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA WAMEFIKISHWA MAHAKAMANI KWA RUSHWA
--
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) leo tarehe 31/3/2016 imewafikisha Mahakamani wabunge watatu ambao ni wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa kosa la kushawishi na kuomba rushwa ya Shilingi Milioni thelathini (30,000,000/-) kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15 (i)(a).
Wabunge hao ni Mheshimiwa Suleiman Ahmed Saddiq Mbunge wa Mvomero;Mheshimiwa Victor Mwambalaswa Mbunge wa Lupa na Mheshimiwa Kangi Lugola Mbunge wa Mwibara.
Wabunge hao wamesomewa shitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mfawidhi, Mh.Thomas Simba.
Akisoma mashtaka hayo wakili wa TAKUKURU, Maghera Ndimbo akishirikiana na Emmanuel Jacob alisema kuwa mnamo Machi 3, 2016 majira ya saa 2 - 4 usiku, katika Hotel ya Golden Tulip iliyopo jijini Dar es Salaam washtakiwa wote watatu waliomba rushwa ya shilingi Mil.30 kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Gairo kwa lengo la kumsaidia ili Taarifa ya Halmashauri hiyo ambayo ilikuwa kwa wakati huo ijadiliwe tahere 16/3/2016 ipitishwe bila marekebisho.
Uchunguzi wa shauri hili bado unaendelea na washtakiwa wote watatu mahakama imewaachia kwa dhamana ya kila mtuhumiwa kuwa na mdhamini mmoja na kulipa shilingi milioni 5. Kesi imeahirishwa hadi tarehe 14/4/ 2016 itakapotajwa tena.
TAKUKURU inawajulisha wananchi wote kwamba hakuna mtu ambaye yupo juu ya Sheria. Rushwa haivumiliki!
IMETOLEWA NA
OFISI YA AFISA UHUSIANO
TAASISI YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA, MAKAO MAKUU
31 MACHI, 2016
Social Plugin