Na Joe Dinga Pefok -Douala, Cameroon
WATU watano wamekamatwa wakituhumiwa kusababisha kifo cha mama mmoja aliyejulikana kwa jina la Monique Koumate na watoto wake mapacha Jumamosi, iliyopita huko Douala nchini Cameroon.
Waliokamatwa ni mkunga wa hospitali hiyo, wauguzi wawili, mhudumu mkuu wa chumba cha kuhifadhia maiti ‘Mortuary’ na mdogo wa marehemu Koumate.
Taarifa za awali zilizotolewa na mashuhuda wa tukio hilo zinaeleza kuwa, mwanzoni Koumate alifikishwa hospitali akiwa katika hali mbaya akisaidiwa na mdogo wake aliyejulikana kwa jina la Agnes.
Wakati mama huyo anafikishwa hospitalini hapo hali yake ilikuwa mbaya na alikuwa kwenye hatua za mwisho za kutaka kujifungua, wahudumu wa afya waliokuwa zamu walikataa kumsaidia kwa sababu hakuwa na pesa kwa ajili ya kulipia huduma.
Agnes alijitahidi kuwasihi wahudumu hao wamsaidie dada yake kwani atawalipa baadaye kwa kuwa hakwenda na pesa lakini waliendeleza msimamo wao kwamba mpaka alipie kwanza ndipo watamsaidia kumzalisha.
Kutokana na kukosa msaada, Koumate alifariki muda mfupi baadaye na baada ya kuona dada yake ameaga dunia, Agnes aliwaomba tena wahudumu hao wamfanyie upasuaji marehemu ili kuwaokoa watoto waliokuwa tumboni ilihali wakisikika kucheza, hivyo ikadhihirisha bado ni wazima lakini wahudumu wale walisisitiza walipwe kwanza ndipo watoe huduma hiyo.
Agnes alichukua jukumu la kuchana tumbo la marehemu dada yake ili aokoe wale watoto mapacha ambapo alifanikiwa kumtoa mtoto wa kwanza akiwa amefariki, wa pili akawa mzima lakini baadaye naye alifariki..
Taarifa zingine kutoka Hospitali ya Laquintinie zilieleza kuwa, Koumate alifikishwa hospitalini hapo akiwa tayari ameshafariki dunia na ndiyo maana mkunga na wahudumu walipuuza kumpeleka wodi ya wazazi.
Wahudumu walieleza kuwa mwili wa marehemu ulitakiwa kupelekwa mochwari lakini Agnes alisisitiza kuwa, mwili wa marehemu dada yake lazima ufanyiwe upasuaji ili kutoa wale watoto.
Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa, Agnes alipuuzia ushauri wa wahudumu na kuamua kupasua tumbo la marehemu dada yake chini ya veranda na kukuta watoto wote wawili wamefariki.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Koumate alikuwa akiishi Douala V na mwanzoni alipelekwa na dada yake kwenye hospitali ya Wialaya ya Nylon huko Douala III na baadaye baada ya hali yake kubadilika ilibidi Agnes amhamishie Hospitali ya Laquintinie ambapo mauti yalimfika.
Au
Social Plugin