Siku mbili baada ya baadhi ya wabunge kudaiwa kuhusika katika vitendo vya rushwa, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola amesema taasisi yake inawahoji wote waliotajwa kuhusika na tuhuma hizo.
Hatua hiyo imekuja kutokana na tuhuma za rushwa dhidi ya wabunge wa baadhi ya kamati za Bunge na kusababisha baadhi yao kuomba kujiuzulu ujumbe wakishinikiza uchunguzi ufanyike ili waliohusika wawekwe hadharani na kuchukuliwa hatua.
Mkuu huyo wa zamani wa Intelijensia ya jinai katika Jeshi la Polisi alisema:“Sisi tunachunguza tuhuma zote zinazohusiana na rushwa, kwa maana hiyo tunawachunguza wabunge wote waliotajwa.”
Alisema uchunguzi huo unakwenda zaidi hadi kuyagusa mashirika ya umma kwa kuwa lengo ni kushughulikia kashfa ambayo inaweza kuharibu heshima ya Bunge.
Mashirika ya umma yaliyoguswa katika tuhuma hizo ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Alipoulizwa uchunguzi huo utakamilika lini, alisema hawezi kubashiri kwa kuwa hilo ni suala la utendaji ambalo linafuata sheria na taratibu.
Wabunge wafunguka
Wakati Takukuru ikichukua hatua hiyo, wabunge watano waliokumbwa na mabadiliko ya kuhamishwa kamati yaliyosababisha baadhi yao kupoteza nyadhifa zao huku yakielezwa kuwa ni ya kawaida, wamefunguka kuhusu uamuzi huo huku baadhi yao wakiushangaa.
Waliopoteza nafasi zao kutokana na mabadiliko hayo ni Richard Ndassa, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji (PIC), Mary Mwanjelwa (Ardhi, Maliasili na Mazingira), Martha Mlata (Nishati na Madini).
Waliovuliwa umakamu mwenyekiti ni Dk Raphael Chegeni (Huduma za Maendeleo ya Jamii) na Kangi Lugola (Hesabu za Serikali za Mitaa).
Mwanjelwa alisema inasikitisha na kushangaza kusikia tuhuma zikitolewa kwenye vyombo vya habari na baadaye kuona mabadiliko ya kamati hizo yakifanyika.
Alisema kwa sasa bado anatafakari: “Lakini kwa kuwa Spika ndiyo amepewa mamlaka kwa mujibu wa kanuni za Bunge basi huwezi kupinga,” alisema.
Mlata alisema kwa sasa hawezi kuzungumza kauli yoyote kabla ya kuonana na Spika.
Ndasa alisema Serikali ina mkono mrefu wa kufuatilia na kuchunguza tuhuma hizo ili kujiridhisha huku akisema mabadiliko yaliyofanyika ni kawaida na yapo ndani ya mamlaka ya Bunge na hawezi kuhusisha mabadiliko hayo na tuhuma za rushwa.
Chegeni alikubaliana na mabadiliko hayo huku akibainisha kuwapo kwa kundi la watu wanaojaribu kuchafua taswira ya kamati yake.
“Mabadiliko ni kawaida tu, anaweza kukupeleka kamati fulani na kukurudisha kamati yako ya zamani na wala siwezi kuhusisha na tuhuma za rushwa, lakini kama kuna rushwa kweli lazima iwe na upande wa mpokeaji na mtoaji, mashirika nayo yachunguzwe na Takukuru kama sehemu ya kuanzia,” alisema.
Zitto Kabwe apongeza
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Zitto Kabwe amepongeza hatua ya TAKUKURU kuanza uchunguzi mara moja ili kurejesha heshima ya bunge.
"Ni hatua muhimu kwamba TAKUKURU imeanza uchunguzi dhidi ya tuhuma za rushwa kwa Wabunge. Ni hatua kubwa itakayopelekea ukweli kujulikana na watakaokutwa na makosa kuchukuliwa hatua stahiki.
Uchunguzi wa vyombo vya dola ni moja ya njia mwafaka ya kuhakikisha kila lisemwalo linakuwa na ukweli na pale ambapo suala limezushwa tu itajulikana na wazushaji hatimaye wataacha.
Pale ambapo itakuwa ni kweli na hatua zikachukuliwa tabia za namna hii zitakoma.
Bila uchunguzi wa kina Bunge litaendelea kugubikwa na kashfa hizi kwa ukweli au kwa hisia.
Hatua iliyochukuliwa na TAKUKURU ni kubwa na ya kuungwa mkono kwa dhati"